• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Walaghai wasiendelee kukosesha taifa mabilioni

TAHARIRI: Walaghai wasiendelee kukosesha taifa mabilioni

Na MHARIRI

UFICHUZI wa Halmashauri ya Kukabiliana na Bidhaa Ghushi Kenya (ACA) kwamba serikali inapoteza Sh200 bilioni kila mwaka kutokana na uingizaji wa bidhaa ghushi nchini unapaswa kuchukuliwa kwa uzito na asasi husika.

Halmashauri hiyo ilionya kwamba mwelekeo huoi ni hatari, kwani kando na kuinyima serikali mapato kupitia kodi, unahatarisha afya ya mamilioni ya Wakenya ambao hutumia bidhaa hizo bila kujua.

Na ijapokuwa Kenya iliungana na dunia nzima jana kuadhimisha Siku ya Kimataifa Kuhusu Bidhaa Ghushi Duniani, kilicho wazi ni kwamba bidhaa hizo zimebaki kuwa tishio kwa Wakenya.

Ni dhahiri kwamba serikali imeongeza kasi ya kukabiliana na bidhaa hizo, hasa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kubuni jopo maalum la kuendesha vita hivyo, ambalo linaongozwa na Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma, Bw Wanyama Musiambo.

Kwa majuma machache ambapo jopo hilo limekuwa likihudumu, tumeona makali ya asasi husika katika kuendesha operesheni hiyo, zinazoongozwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i.

Licha ya juhudi hizi, linalojitokeza ni kwamba ingawa mkakati huo unaonekana kuwa madhubuti, una upungufu, kwani hauna sera au utaratibu ambao utaendesha harakati hizo kwa muda mrefu.

Kwanza, sheria zilizopo hazijaelezea mpango huo kiwazi; moja likiwa adhabu wanazopaswa kupewa watu ambao wanapatikana kushiriki katika vitendo hivyo.

Pengo hilo la kisheria pia linajumuisha ukosefu wa faini na vifungo vinavyopaswa kutolewa kwa wahusika hao.

Katika kujitetea kwake, serikali iliahidi kupanua ushirikiano wa kiasasi, kwa kushirikisha Polisi wa Kimataifa (Interpol) na ubalozi wa nchi kama Amerika na Uingereza, ili kuwanasa watu hao, hasa katika maeneo ya mipakani.

Kwa hayo, ombi letu ni kwa serikali kudumisha mikakati hiyo, kwa kuhakikisha kwamba vita hivyo haviendeshwi kwa muda fulani, ila vinakumbatiwa na kutekelezwa kama mojawapo ya sera kuu za serikali.

Hili ni tatizo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu, hivyo lazima suluhisho lake liwe mkakati utakaotoa utatuzi wa kudumu. Lazima asasi husika zishirikishwe kikamilifu ili kuziendesha kwa pamoja.

Ni kupitia hatua kama hizo ambapo manufaa kamili yatapatikana.

You can share this post!

Polo akemea mke kwa kuomba chumvi kwa dume jirani

FUNGUKA: Lengo langu ni kupata zaidi ya watoto 9

adminleo