• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:50 AM
MAREKEBISHO YA KATIBA: Raila achokoza Jubilee

MAREKEBISHO YA KATIBA: Raila achokoza Jubilee

KITAVI MUTUA na VALENTINE OBARA

MSIMAMO wa Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa alikubaliana na Rais Uhuru Kenyatta kutakuwa na marekebisho ya Katiba walipoweka muafaka wa maelewano hapo Machi 9, huenda ukaibua upya mgogoro katika chama cha Jubilee.

Wakati Bw Odinga alipotoa pendekezo hilo wiki chache baada ya muafaka wake na Rais Kenyatta, kulizuka mvutano ndani ya Jubilee ambapo mrengo mmoja ukiongozwa na Naibu Rais William Ruto na wandani wake akiwemo Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale ulipinga vikali.

Mjadala huo ulipokuwa ukiendelea Rais Kenyatta alikuwa kimya hadi mwishowe akajitokeza na kusema hakuna muda wala rasilimali za kuandaa kura ya maamuzi ya kufanyia marekebisho Katiba.

“Hakuna nia yoyote ya kurekebisha katiba. Hatuna wakati. Tunataka kufanya kazi muhimu, sio kukimbia hapa na pale kuuliza kama mnataka Katiba mpya au la. Hilo halitatatua matatizo yetu,” akasema rais alipozungumza mwezi Mei katika Ikulu ya Nairobi.

Msimamo huo wa rais unakinzana na ule wa Bw Odinga ambaye amesisitiza walikubaliana suala hilo litakuwa moja ya ajenda kuu za maelewano yao.

Bw Ruto hakuhusishwa kwenye muafaka huo na baadhi ya wandani wake wana wasiwasi kuhusu kile wawili hao walikubaliana kwenye maelewano yao.

Akizungumza katika Kaunti ya Kitui, Bw Odinga alisisitiza ni lazima Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuleta mabadiliko Kenya.

“Tulikubaliana na Rais Kenyatta kwamba tukifanikiwa kurekebisha makosa yaliyo kwenye Katiba tutakuwa tumefanikiwa kuleta mabadiliko Kenya kwa hali ambayo itafanya liwe taifa bora zaidi kwa vizazi vijavyo,” akasema.

Kiongozi huyo alisema Katiba iliyopo, ambayo ilipitishwa mwaka wa 2010, imedhihirisha haiwezi kutatua changamoto nyingi zinazokumba taifa hili.

Miongoni mwa marekebisho anayotaka ni kuhusu mfumo wa uongozi ili kuwe na ngazi tatu za utawala, tofauti na jinsi ilivyo sasa ambapo kuna ngazi mbili ambazo ni Serikali Kuu na za kaunti.

Kulingana naye, muafaka ulipatikana kati yake na rais baada yao kukubaliana kuwa marekebisho ya Katiba yatakuwa kati ya masuala makuu yatakayoangaziwa.

“Tuna Katiba nzuri lakini haitusaidii. Hii ndio sababu nilishirikiana na Rais Kenyatta ili kufanya marekebisho ya kisheria,” akasema.

Mtaalamu wa kisheria ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu wa uundaji wa Katiba iliyopo, Bw Nzamba Kitonga, alisema wakati huu ni mwafaka kwa Katiba kufanyiwa marekebisho.

Kulingana naye, kamati yake ilikuwa imetarajia Katiba itahitaji marekebisho baada ya miaka saba au kumi.

Lakini wandani wa Bw Ruto wamekuwa wakishikilia kuwa marekebisho ya kikatiba ni njama fiche ya Bw Odinga kumharibia nafasi ya kushinda urais 2022.

Jopokazi lililoteuliwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga limekuwa likiendeleza shughuli zake kichinichini na kufikia sasa haifahamiki hatua zilizopigwa katika majukumu yao.

Bw Odinga alisema marekebisho ya Katiba ni miongoni mwa yanayoangaziwa na jopokazi hilo, ambalo kulingana naye litaanza kuzuru maeneo tofauti ya nchi hivi karibuni kutafuta maoni ya wananchi.

Alisema baadhi ya maswali ambayo wananchi wataulizwa ni kuhusu jinsi ugatuzi unavyoweza kuimarishwa, mbinu mwafaka za ugavi wa rasilimali za nchi na kama wanataka mfumo uliopo wa uongozi uendelee kutumiwa au ubadilishwe.

You can share this post!

Wakenya wakerwa na wabunge kulipiwa mamilioni kutazama...

Wanafunzi watundu watajua hawajui – Belio Kipsang

adminleo