• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Saa rasmi za masomo ni 8.00 asubuhi hadi 3.30 alasiri – Amina Mohamed

Saa rasmi za masomo ni 8.00 asubuhi hadi 3.30 alasiri – Amina Mohamed

NA CHARLES WASONGA

SAA za masomo sasa zitaanza saa mbili asubuhi na kukamilika saa tisa na nusu jioni, serikali imeamuru. 

WAZIRI wa Elimu Amina Mohamed Jumanne alitoa agizo hilo jipya ambalo litaathiri shule zote nchini na ambalo litaanza kutekelezwa mara moja.

“Kuanzia sasa masomo shule yataendeshwa kuanzia saa mbili asubuhi na saa tisa na nusu jioni. Amri hii itawezesha wanafunzi kupata muda wa kupumzisha akili zao na kupunguza hali ya sasa ambapo baadhi ya wanafunzi wanalalamika kuzongwa na kazi nyingi,” Bi Mohamed akasema.

Waziri alisema mipango mingine yoyote ya kuwalazimisha wanafunzi kuwasilisha shuleni kabla ya saa mbili asubuhi na saa tisa na nusu jioni itakuwa kinyume cha sheria.

Waziri Mohammed alitoa amri hiyo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Elimu kuwasilisha ripoti kuhusu visa vya utovu wa nidhamu vilivyokithiri shule katika muhula huu wa pili.

Katika ripoti yake waziri anasema kuwa jumla ya visa 107 vya utovu wa nidhamu viliripotiwa katika shule za umma za upili kote nchini. Kesi nyingi ziliripotiwa katika maeneo ya Mashariki, Rift Valley na Nyanza vikiandikisha visa 40, 25 na 20, mtawalia.

Alisema visa 63 kati ya hivyo vilihusu uchomaji wa mali ya shule hasa mabweni eneo la Kati ikiongoza kwa visa 22 ikifuatwa na Nyanza ambako shule 17 ziliathirika. Visa vingine vilikuwa ni fujo na uharibifu wa mali na wanafunzi kususia masomo.

Waziri Mohammed jana aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Elimu kwamba visa hivyo vilivyopelekea shule nyingi kufungwa, vilitokana na wanafunzi kuogopa mitihani ya mwigo na ile ya kitaifa.

“Visa vingi vya fujo na uchomaji wa shule vilisababishwa na wanafunzi wa kidato cha nne ambao waliingiwa na hofu ya kufeli mitihani baada ya wizara yangu kuweka mikakati kali ya kuzuia wizi wa mitihani,” akasema.

“Mwana wangu wa kiume aliwahi kunilaumu kwa kukosa kumsaidia kuiba mtihani ilia pate alama ya A katika mtihani wa kidato cha nne (KCSE) ya 2015. Hii ni kutokana na dhana kwamba wanafunzi wengine walikuwa wakisaidia kupita mitihani,” Bi Mohammed aliwaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melly.

Aliongeza kuwa baadhi ya wanafunzi walizua fujo kutokana na uhaba wa walimu na vifaa vya masomo, matumizi ya mihadarati, usimamizi mbaya shule na hulka ya kuiga wenzao watundu na hali ya walimu kutoweza kukamilisha silabasi.

“Sikubaliani na kauli ya vyama vya walimu nchini, Knut na Kuppet kwamba tatizo hili lilichangiwa na hatua ya Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuwahamisha walimu wakuu mapema mwaka huu,” akasema.

Knut imetisha kuitisha mgomo mwezi Septemba kupinga uhamisho wa walimu wakuu na agizo la walimu kutakiwa kutia jaza fumo za kutathmini utendakazi wao kila mara.

Mbunge Maalum Wilson Sossion, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Knut alishikilia kuwa nyingi za shule ambazo ziliathiriwa ni zile ambazo walimu wao wakuu walikuhamishiwa shule zingine.

“Shule za Kitaifa kama vile Maranda na Friends Schools Kamusinga ni miongoni mwa shule ambazo zilishuhudia fujo mwaka huu baada ya walimu wao wakuu kuhamishwa,” akasema Bw Sossion.

Lakini Bi Mohammed alijibu kwa kusema kuwa alizuru shule nyingi katika muhula huu wa pili na kutambua kuwa uhamisho wa walimu haukusababisha tatizo hilo. “Nilizuru shule za upili za Kakamega na Alliance, kati ya shule nyinginezo nikapata masomo yakiendelea kwa njia bila shida yoyote. Shule hizi ni miongoni mwa 155 ambazo walimu wao wakuu walihamishwa mwanzoni mwa mwaka huu,” akasema.

Waziri Mohammed alisema kufikia jumla ya wanafunzi 198 wamekamatwa kote nchini kwa kuzua ghasia na kusababisha uharibifu wa mali shuleni mwao.

You can share this post!

Mwana mpotevu atarudi nyumbani?

Kibe alishinda kwa njia ya haki – Mahakama

adminleo