• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 8:55 AM
Ziara ya ghafla ya Rais Kenyatta kaunti ya Lamu

Ziara ya ghafla ya Rais Kenyatta kaunti ya Lamu

NA KALUME KAZUNGU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano alifanya ziara ya ghafla kaunti ya Lamu ambapo alikagua miradi mbalimbali inayoendelezwa na serikali kuu eneo hilo.

Akiwa ameandamana na Waziri wa Uchukuzi, James Macharia, Mkuu wa Majeshi nchini, Samson Mwathethe na maafisa wengine wakuu serikalini, Rais Kenyatta alitembelea eneo kunakojengwa mradi wa Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET) huko Kililana, ambapo alikutana na maafisa wakuu wanaosimamia mradi huo na kuwahimiza kuharakisha ujenzi wa bandari hiyo.

Ujenzi wa viegesho vitatu vya kwanza vya LAPSSET unaendelea na uko asilimia 52 kukamilika, ambapo kiegesho cha kwanza kinatarajiwa kukamilika kufikia Disemba mwaka huu.

Rais Kenyatta akikagua barabara ya mji wa Mokowe ambayo ilijengwa kupitia halmashauri ya Ujenzi wa barabara za maeneo ya miji nchini (KURA). Picha/ Kalume Kazungu

Rais Kenyatta pia alikagua mradi wa barabara kuu ya Lamu hadi Garsen.

Barabara hiyo ya urefu wa kilomita 135 inajengwa na kampuni ya H-Young.

Rais pia alikagua mradi wa barabara ya kilomita 15 ya mji wa Mokowe ambayo inajengwa kupitia ufadhili wa Halmashauri ya Usimamizi wa Barabara za Maeneo ya Miji (KURA).

Wakati wa ziara hiyo, Rais Kenyatta alitoa makataa ya mwaka mmoja kwa baadhi ya wanakandarasi kuhakikisha wamekamilisha miradi yao.

-Rais Uhuru Kenyatta akiwa ameandamana na Waziri wa Uchukuzi, James Macharia na Mkuu wa majeshi nchini, Samson Mwathethe wakati wakikagua miradi ya serikali ya kitaifa kaunti ya Lamu Juymatano Agosti 1, 2018. Picha/ Kalume Kazungu

Akigusia kuhusu barabara ya Lamu kuelekea Garsen, Rais Kenyatta alieleza kusikitishwa kwake na jinsi ujenzi wa barabara hiyo unavyotekelezwa kwa upole mwingi.

Alimtaka mwanakandarasi anayejenga barabara hiyo kuharakisha, akiitaja barabara hiyo kuwa muhimu si kwa wakazi wa Lamu pekee bali pia kwa usalama wa eneo hilo.

Pia aliamuru ujenzi wa barabara zinazounganisha Lamu na maeneo ambako mradi wa LAPSSET unaendelezwa kuharakishgwa.

‘Itakuwaje tuko na mradi mkubwa kama bandari ya Lamu (LAPSSET) na hatuna barabara nzuri zinazounganisha eneo hilo. Lazima barabara za kuelekea eneo la LAPSSET zijengwe kwa haraka ili iwe rahisi kufikia eneo hilo. Pia barabara ya Lamu hadi Garsen ijengwe kwa haraka. Barabara hii si muhimu tu kwa wakazi wa Lamu pekee bali pia itaimarisha usalama wa eneo hili,’ akasema Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta akiklagua ujenzi wa barabara kuu ya Lamu hadi Garsen katika eneo la Hindi, Kaunti ya Lamu. Aliagiza ujenzi wa miradi hiyo kutekelezwa kwa haraka. Picha/ Kalume Kazungu

Waziri wa Uchgukuzi, James Macharia, aliahidi kuhakikisha kuna usimamizi bora katika kutekelezwa kwa miradi hiyo hasa ujenzi wa barabara za Lamu.

Viongozi wa Lamu waliokutana na Rais aidha walitaja ziara yake kuwa muhimu kwani itabadilisha hali ya mambo eneo hilo.

‘Ninaamini ziara ya Rais wetu eneo hili itawatia uwoga baadhi ya wanakandarasi ambao hawajawajibikia kazi zao,’ akasema Bi Anab.

Ziara ya Rais Kenyatta inajiri wakati ambapo wakazi na viongozi wa Lamu wamekuwa wakiilalamikia kampuni inayoendeleza ujenzi wa barabara kuu ya Lamu hadi Garsen kwa utepetevu mwingi kazini.

You can share this post!

Walioingiza wasichana wa Nepal nchini kunengua viuno...

ULIMBWENDE: Jinsi ya kuondoa weusi makwapani

adminleo