• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
MLIPUKO WA BOMU 1998: Mwito wa amani kwenye kumbukumbu

MLIPUKO WA BOMU 1998: Mwito wa amani kwenye kumbukumbu

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI za Kenya na Amerika Jumanne zilikariri kujitolea kwao kushirikiana kupambana na ugaidi, miaka 20 baada ya mlipuko wa bomu uliotekelezwa na kundi la kigaidi la Al-Qaeda katika ubalozi wa Amerika jijini Nairobi mnamo Agosti 7, 1998.

Akizungumza kwa niaba ya serikali, Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi (NCTC), Bw Martin Kimani, alisema ingawa Kenya imepiga hatua kubwa katika kupambana na mashambulio ya kigaidi, bado tishio hilo lipo.

“Tishio la ugaidi bado lipo na inahitajika tuzidi kuwa macho. Kuendelea mbele, ni lazima tukumbatie tofauti zetu iwe ni za kidini, kikabila au kitamaduni. Hatua hii itanyima magaidi nafasi ya kutumia tofauti zetu kutekeleza mipango yao ya mashambulio,” akasema.

Alikuwa akizungumza katika kwenye hafla ya kumbukumbu za shambulio la 1998 jijini Nairobi.

Wito sawa na huo ulitolewa na Balozi wa Amerika nchini, Bw Robert Godec ambaye aliongeza kuwa magaidi hawatakubaliwa kuvuruga amani.

“Ingawa magaidi walitaka kuleta hofu na mgawanyiko, walishindwa. Badala yake, tuliinuka tukiwa na maazimio makubwa zaidi ya kushirikiana kukuza uhuru, haki na amani,” akasema balozi huyo ambaye wakati huo alikuwa mmoja wa wafanyakazi katika ubalozi huo.

Wakati wa hafla hiyo, kulikuwa na filamu iliyoonyesha baadhi ya waathiriwa wakieleza jinsi maisha yao yalivyoathirika baada ya mkasa huo uliosababisha vifo vya watu karibu 250 na kujeruhi maelfu wengine.

Miongoni mwa waliojeruhiwa ni aliyekuwa Waziri wa Elimu, Bw Joseph Kamotho, na aliyekuwa Balozi wa Amerika nchini, Bi Prudence Bushnell, ambao walikuwa mkutanoni katika jengo hilo la ubalozi.

“Ilikuwa kama jehanamu. Jengo liliporomoka, magari yalikuwa yanachomeka, mamia ya watu walikuwa juu ya Jumba la Ufundi wakijaribu kutafuta manusura,” akaeleza.

Bw Joash Okindo ambaye alikuwa mmoja wa walinzi wakuu wa ubalozi huo, alieleza jinsi magaidi walivyowasili kwa gari la manjano ambalo halikuwa na nambari za usajili.

“Mmoja wao alishuka akaja kuongea nami kuniambia nifungue geti. Nilikataa kufungua nikamwambia kama hamtaondoka hapa nitawaua. Alisema sawa, niue, nilizaliwa mara moja na kifo pia ni cha mara moja,” akasema.

Alieleza jinsi alivyojaribu kupigia maafisa wa usalama wa ubalozi huo simu lakini simu zote alizopiga zilikuwa zinatumika.

Bi Esther Njeri, ambaye alipoteza fahamu katika mkasa huo, alisema alipitia maisha magumu kulea wanawe wawili kufuatia majeraha aliyopata yaliyomfanya kukosa ajira.

Hata hivyo, aliongeza kuwa anashukuru Mungu kwa kuwa mmoja wao sasa anafanya kazi katika benki na mwingine amefuzu na shahada ya uwakili.

Kwa upande wake, Bw Douglas Sidialo ambaye alipoteza uwezo wa kuona sasa hujihusisha katika mashindano ya uendeshaji baiskeli ambayo yamempa umaarufu kimataifa.

“Tangu siku hiyo, sijawahi kuona mwangaza maishani mwangu. Nilipotoka hospitalini nilikuwa na hasira sana. Nilisema kama ningekutana na hao magaidi, ningewachuna ngozi wakiwa hai. Lakini baadaye niligundua hasira haisaidii,” akasema.

You can share this post!

NYS: Agizo DPP atenganishe kesi kumi mara tatu

Hofu baada ya wanaume kuonywa na vijana watatahiriwa

adminleo