• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:10 AM
WANDERI: Nafasi ya waliosoma katika jamii i wapi?

WANDERI: Nafasi ya waliosoma katika jamii i wapi?

Na WANDERI KAMAU 

UWEKEZAJI katika elimu ndiyo ulizifanya nchi kama Ugiriki na Roma kustawi sana katika masuala muhimu kama historia, sayansi na uvumbuzi hadi sasa.

Nchini Ugiriki, kulikuwa na mpango ambapo, wale ambao walioonekana kuwa werevu walipelekwa katika Kituo Maalum cha Mafunzo ambacho kiliongozwa na wanafalsafa Plato, Socrates na Aristotle. Mpango huo ndio uliozaa Chuo Maalum cha Kifalsafa cha Plato, maarufu kama Platonic Academy.

Ni mikakati kama hiyo iliyopelekea Ugiriki kuwa miongoni mwa nchi ambazo zinaheshimiwa zaidi katika uwanda wa falsafa, hadi sasa.

Zaidi ya hayo, elimu ilipelekea Ugiriki pia kupata hekima kubwa katika masuala ya kidini, kwani ilikuwa na mpangilio maalum wa miungu wake.

Kinachojitokeza ni kwamba, Ugiriki iliwekeza sana katika elimu, kumaanisha kwamba, wale ambao walisoma walipewa nafasi na umuhimu mkubwa sana katika jamii.

Hata hivyo nchi za Afrika zimeenda kinyume na mwelekeo huo, hali ambayo imezifanya kubaki nyuma katika masuala muhimu ya kielimu.

Hii ni licha ya misingi ya sera zake kuweka msisitizo mkubwa katika masuala ya elimu, sayansi na uvumbuzi mara tu baada ya kujinyakulia uhuru.

Kwa mfano, Kenya ilibuni sera maalum ya kupiga teke ujinga na hali ya kutojua miongoni mwa raia wake, ili kuhakikisha kwamba wanafahamu mielekeo ya kisasa ya elimu na sayansi.

Ni kwa hayo ambapo Mzee Jomo Kenyatta alitilia mkazo sana masuala ya elimu, kwani yeye mwenyewe alikuwa mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Walimu ya Thogoto, katika Kaunti ya Kiambu.

Hata hivyo, msisitizo huo umebadilika, kwani kwa sasa, ni dhahiri kwamba waliosoma hawana nafasi yoyote katika jamii ya sasa.

Kinaya ni kuwa, badala ya kupewa nafasi muhimu ya kuihudumia jamii, wamegeuzwa kuwa vinyago wa kuchekwa, hasa na wale walioajiriwa kwa kughushi karatasi zao za masomo.

Mfumo wa uajiri katika taifa hili umebadilika na kugeuzwa kuwa chemichemi ya ‘kuwazawadi’ washirika wa karibu wa wakuu wanaoongoza idara husika.

Katika Kenya ya sasa, si vigumu kumkuta mtu aliyesoma hadi kiwango cha shahada ya uzamifu (PhD) au uzamili (Masters) akiwa hana ajira, ilhali vibaraka wa kiongozi fulani ama mkuu wa idara wanapokea mishahara minono bila viwango vyovyote vya masomo.

Kule ambako hali hii imekithiri ni katika serikali ya kitaifa, serikali za kaunti na mashirika ya kibinafsi.

Katika serikali za kaunti, si nadra kuwaona magavana wakiwaajiri jamaa zao katika nafasi za hadhi kwa msingi wa kudhihirisha kwamba wao “ndio viongozi.”

Katika mashirika ya kibinafsi, mfumo wa kuwaajiri ama kuwapandisha kazi wafanyakazi huwa mambo ya kisiri ambayo hufanyiwa gizani.

Hakuna taratibu zozote ambazo hutolewa; ila matokeo huwa “Mwafulani kapandishwa ngazi” au “Mwafulani kaajiriwa”-ilmradi huwa ni mambo ya kisiri yasiyo uwazi wowote.

Matokeo huwa ni kudorora kwa mfumo wa uwazi na udunishaji wa bidii za waliosoma.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ifikirie tena juu ya ushuru mpya

Kipute cha voliboli ya walemavu kuanza Makueni

adminleo