• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:25 PM
GWIJI WA WIKI: Mfahamu mwanafasihi Mukoya Aywah

GWIJI WA WIKI: Mfahamu mwanafasihi Mukoya Aywah

Na CHRIS ADUNGO

NASAHA

Huu ndio ushauri, walimwengu fahamuni,

Epukana na kiburi, mkaishi salamani,

Shikilia ujasiri, nawambia mioyoni.

Muweke mbele ilimu, ndo uhai wa maisha,

Kipaji pia muhimu, usitarabu onyesha,

Ukakamavu fahamu, busara nyingi zidisha.

KUFAULU katika maisha ni zao la imani, bidii, ubunifu, nidhamu na stahamala. Badili mtazamo wako kuanzia sasa na amini kwamba ipo miujiza na nguvu kubwa ajabu katika kuamini. Jifunze kushinda hofu na amini katika ushindi. Kujiamini ni mwanzo mwema katika kulijaribu jambo lolote duniani.

Huu ndio ushauri wa Bw Hezekiah Mukoya Aywah – mtunzi mahiri wa mashairi, mpenzi kindakindaki wa Taifa Leo, seremala hodari, mwigizaji shupavu na bingwa wa masuala ya filamu ambaye kwa sasa ni mtetezi mkubwa wa Kiswahili, mwanaharakati wa haki za binadamu na wanyama; na pia Meneja wa Mauzo katika Kundi la Sanaa la Miale ya Njiwa Theatre Production, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Aywah alizaliwa mnamo Oktoba 23, 1994 katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu akiwa mtoto wa tatu kati ya wanne katika familia ya Bi Irene Shieyo Mzungu na Bw Edward Mukoya.

Baada ya kupata elimu ya chekechea katika iliyokuwa Shule ya Malezi, eneo la Kiandutu mjini Thika kati ya 1999-2000, Aywah aliyelelewa na mama wa kambo, alijiunga na Shule ya Msingi ya Garissa Road, Thika alikosomea hadi mwisoni mwa Darasa la Pili mnamo 2002.

Mnamo 2003, Aywah aliungana na mamaye mzazi katika mtaa wa Kibra, Nairobi na kujiunga na Shule ya Msingi ya St Augustus, alikosomea kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee kabla ya kuelekea katika Shule ya Msingi ya Lang’ata Road mwanzoni mwa 2004 akiwa mwanafunzi wa Darasa la Nne.

Aywah anatambua ukubwa na upekee wa mchango wa aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Lang’ata Road Primary, Bw Njoroge katika kumwelekeza vilivyo, kumtia katika mkondo wa nidhamu kali, kumhimiza na kumshajiisha zaidi kujitahidi masomoni akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Mnamo Mei 2007, Aywah alijeruhiwa vibaya na kakaye baada ya ugomvi uliozua vita vikali baina yao. Alilazwa na kutibiwa kwa miezi kadhaa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Nairobi.

Baada ya kupata nafuu, alirejea mjini Thika kuishi na baba mzazi na kujiunga na Shule ya Msingi ya King Solomon Academy katika eneo la Kiganjo.

Ingawa alama alizozipata katika mtihani wa KCPE mwishoni mwa 2009 zilimpa nafasi katika Shule ya Upili ya Philadelphia Mixed Boarding, Murang’a, uchechefu wa karo ulimweka katika ulazima wa kujiunga na Shule ya Upili ya Broadway, Thika.

Aywah anaamini kwamba Kiswahili kwa sasa kimekua sana kiasi cha kutumiwa kuendeshea shughuli zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika. Picha/ Chris Adungo

UIGIZAJI

Japo kujiunga kwake na Broadway kulitarajiwa kumfungulia milango ya heri katika safari ya elimu, jambo ambalo lilikuwa mbali kabisa na ufahamisho wa Aywah ni ukweli kwamba hapo ndipo angekutana baadaye na Bw James Mbothu, mwalimu aliyempokeza malezi bora zaidi katika sanaa ya uigizaji.

Bw Mbothu ambaye kwa wakati huo alikuwa msimamizi wa masuala ya drama na muziki shuleni Broadway, kwa sasa ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya Upili ya Gaichanjiru Boys, Murang’a.

Mbali na kupanda mbegu zilizootesha mapenzi ya dhati kwa Kiswahili ndani ya moyo mchanga wa Aywah, Bw Mbothu alimchochea mwanafunzi wake huyo kushiriki mashindano mbalimbali ya tamasha za muziki na drama hadi kufikia kiwango cha kitaifa.

Chini ya ulezi wake, Aywah alidhihirisha utajiri mkubwa wa kipaji cha uigizaji, ulumbi na uimbaji. Upekee huo ndio uliompandisha Aywah kwenye majukwaa mengi ya tuzo mbalimbali za haiba kubwa katika sanaa ya drama.

Baada ya kuibuka kidedea katika mashindano ya utambaji wa hadithi miongoni mwa wanafunzi wa shule za upili katika uliokuwa Mkoa wa Kati, Aywah alidhaminiwa na Benki ya Equity kusomea kozi ya mwaka mmoja katika masuala ya uchumi mnamo Oktoba 14, 2011.

Mashairi aliyoyaghani, nyimbo alizozitunga, hotuba alizozitoa, mijadala aliyoishiriki, hadithi alizozitamba na michezo aliyoiigiza akiwa mwanafunzi shuleni Broadway kuanzia Februari 2010 ilimvunia Aywah umaarufu miongoni mwa walimu na wanafunzi wenzake, tija belele na mataji ya kuonewa gere.

Kilele cha usanii wake akiwa mwanafunzi wa shule ya upili ni kutambuliwa kwa jitihada zake na vinara wa kampuni ya Broadway Bakery ambao kwa ushirikiano na aliyekuwa Mkuu wa Elimu katika Kaunti ya Kiambu, walimtuza pakubwa.

Hii ilikuwa baada ya Aywah kuibuka bingwa wa kitaifa wa Kitengo cha Mashairi katika tamasha za kitaifa za muziki na drama kwa shule za upili mnamo 2012-13.

 

MIALE YA NJIWA

Aywah alifanya mtihani wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) shuleni Broadway High mwishoni mwa 2013 kisha akajiunga na Miale ya Njiwa Theatre Production, Nairobi waliompiga msasa zaidi katika masuala ya uigizaji hadi Aprili 2014.

Ubora wa kiwango chake katika sanaa ni kiini cha Miale ya Njiwa chini ya usimamizi wa Bw Anthony Chege, kumteua kuwa Meneja wa Mauzo miezi michache baadaye.

Kufikia sasa, Aywah anajivunia kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili na kushirikiana na wenzake kuigiza vitabu teule vya fasihi vinavyotahiniwa katika kiwango cha mtihani wa KCSE.

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kusomea uanahabari na pia kuwa mzalishaji maarufu zaidi wa filamu za ushairi wa Kiswahili, Aywah anashikilia kwamba mwangwi wa kusisitiza umuhimu wa uzalendo, maadili, elimu na uongozi bora kupitia matumizi fasaha ya Kiswahili, ni jambo ambalo amepania kuliakisi katika usanii wake.

Mnamo 2013, alijitosa pia katika ulingo wa useremala baada ya utajiri wa kipaji hicho kuanza kujikuza ndani yake tangu akiwa tineja. Tangu 2015, Aywah amekuwa seremala katika kampuni ya Kevian Ltd, Thika inayotengeneza sharubati na vinywaji vingine visivyolevya.

 

USHAIRI

Kwa imani kwamba wasanii wana nafasi kubwa katika kuchangia makuzi ya lugha, utamaduni na mawasiliano; nafasi ya Kiswahili ni miongoni mwa dhamira muhimu zinazojadiliwa na Aywah katika mengi ya mashairi yake ambayo huchapishwa na Taifa Leo na Taifa Jumapili aghalabu kila wikendi.

Si ajabu kuelewa kina cha huzuni, ukiwa na fadhaa ya Aywah kila anapokutana na yeyote anayekiponda Kiswahili au kukisema ovyo bila ya kuzingatia usahihi wa sarufi ya lugha yenyewe.

Aywah anaamini kwamba Kiswahili kwa sasa kimekua sana kiasi cha kutumiwa kuendeshea shughuli zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Afrika.

Kinachomtofuatisha Aywah na washairi wengine chipukizi, ni upevu wake katika umilisi wa Kiswahili na upana wa ujuzi alionao katika kufumbata ujumbe kwa kutumia tamathali mbalimbali za usemi.

You can share this post!

KAULI YA WALIBORA: ‘Shosho’ Cecilia ni mfano hai kuwa...

Kaunti nyingi bado hazijafikia viwango vya IMF –...

adminleo