• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Haji aje bungeni awakamate wabunge waliomeza hongo ya Sh10,000 – Wabunge wa Magharibi

Haji aje bungeni awakamate wabunge waliomeza hongo ya Sh10,000 – Wabunge wa Magharibi

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE kutoka eneo la magharibi sasa wanamtaka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kuendesha uchunguzi bungeni wakidai asasi hiyo imezongwa na visa vya wabunge kupokea hongo ili kuhujumu vita dhidi ya ufisadi.

Wakiongea na wanahabari Alhamisi jioni baada ya kukataliwa kwa ripoti kuhusu sakata ya sukari, wabunge hao walidai wafanyabiashara matajiri wa sukari “waliwanunua” wabunge ili waangushe ripoti hiyo.

Mbunge wa Matungu Justus Murunga alidai kuwa wabunge waliopinga ripoti hiyo iliyowaelekezea lawama mawaziri Henry Rotich (Fedha), Adan Mohammed (Masuala ya Afrika Mashariki) na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Willy Bett, walihongwa kwa kati ya Sh10,000 hadi Sh30,000.

Aliandamana na wenzake Ayub Savula (Lugari), Tindi Mwale (Butere), Catherine Wambilianga (Mbunge Mwakilishi wa Bungoma), Benard Shinali (Ikolomani), Simba Arati (Dagoreti Kaskazini), Godfrey Omuse (Teso Kusini), Onyango K’Oyoo (Muhoroni), Godffrey Osotsi (maalum, ANC) na Joyce Kamene (Mbunge Mwakilishi wa Machakos).

“DPP anafaa kuja bungeni kwa haraka na kuanzisha uchunguzi. Kile tulishuhudia ni aibu, inatamausha na ni hatari kwa ustawi wa nchi,” akasema Bw Savula, akirejelea matukio ambapo baadhi ya wabunge walikuwa wakiwapokeza wenzao bahasha zenye pesa.

Kwa upande wake Bw Arati alisema aliowaona wabunge wenzake wakihongwa waziwazi kuwashawishi kutupilia mbali ripoti hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya pamoja chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Kieni Kanini Kega na mwenzake wa Mandera Kusini Adan Haji.

“Leo nimewaona wazi wabunge ambao hupokea mishahara ya jumla ya Sh1 milioni wakihongwa kwa Sh10,000 ili watupilie mbali ripoti kama hii yenye umuhimu mkubwa kwa taifa. Hii ina maana kuwa Wakenya wataendelea kununua sukari yenye sumu huku wakulima wa miwa wakiendelea kutesa kufuatia kuporomoka kwa kampuni za miwa,” akasema Bw Arati.

Bw Mwale alisema ni kinyume cha sheria kwa wabunge ambao wametwikwa jukumu la kutunga sheria wakivuinja sheria hiyo kwa kushiriki rushwa.

“Katiba ya sasa na sheria zingine husika kuhusu vita dhidi ya ufisadi zilipitishwa hapa bungeni. Sasa inakuaje kwamba watu ambao walipitisha sheria hizo wanageuka tena na kuzivunja kiholela? Tunatoa mfano gani kwa Wakenya na haswa watoto wetu walioko shuleni? Akauliza Bw Mwale.

Wabunge ambao walitupilia mbali ripoti hiyo waliongozwa na kiongozi wa wengi Aden Duale na mwenzake wa wachache John Mbadi, wote wakilenga kuwalinda Mbw Rotich na Mohammed.

You can share this post!

Waliobomolewa majengo Nairobi walete vibali – Polisi

Ni heri nipoteze marafiki nikiokoa Wakenya – Uhuru

adminleo