• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Gor yahitaji Sh8 milioni kuwajibikla mechi za CAF

Gor yahitaji Sh8 milioni kuwajibikla mechi za CAF

Na CECIL ODONGO

MABINGWA mara 16 wa KPL Gor Mahia wanahitaji kima cha Sh 8 milioni ili kugharamia mechi mbili za awamu ya makundi ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho Barani Afrika, CAF.

K’Ogalo wanatarajiwa kuwa wenyeji wa mabingwa wa ligi ya Rwanda, Rayon Sports Agosti 19 kabla ya kusafiri hadi Algeria kuwajibikia mechi yao ya mwisho awamu ya makundi dhidi ya USM Algiers Agosti 29.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Omondi Aduda, klabu hiyo itahitaji kiasi hicho cha hela ili kucheza mechi hizo mbili.

“Tunaiomba serikali itusaidie kukamilisha mechi zetu mbili za CAF za awamu ya makundi. Tunahitaji Sh3 milioni katika mechi ya nyumbani dhidi ya Rayon Sports na Sh 5.6 milioni kucheza mechi ya ugenini dhidi ya USM Algiers,” akasema Bw Aduda.

Afisa huyo alisema kwamba kwa kuwa mabingwa hao wanawakilisha taifa itakuwa jambo la busara iwapo serikali itaingilia kati kugharimia fedha za kuwa wenyeji wa Rayon Sports na pia tiketi za kusafiria Algeria.

“Sisi ndiyo wakulipia uwanja wa mazoezi utakaotumiwa na wapinzani wetu, tiketi za usafiri kwa marefa wa mechi hiyo kutoka Zimbabwe na msimamizi mkuu wa mechi,” akasema Bw Aduda.

Kando na hilo K’Ogalo watahitajika kulipa Sh500,000 za kupata visa kwa kila mchezaji na afisa wa timu atakayesafiri na tiketi ya Sh 130,000 za ndege aina ya Turkish Airline kwa kila msafiri.

Aidha alifichua kwamba tayari wametumia zaidi ya nusu za mgao wa fedha kutoka CAF zilizolenga kugharimia na kudhamini mechi hizo na pesa zilizosalia haziwezi kuyakimu mahitaji katika mechi hizo mbili.

“Tulitumia pesa hizo kulipia gharama za mechi ya Yanga na USM Algiers na pia tukatumia pesa hizo kwa malipo ya malazi na tiketi tuliposafiri Rwanda kwa mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Rayon Sports,” akaongeza Bw Aduda.

Gor Mahia kwa sasa wanashikilia uongozi wa kundi hilo la D na iwapo watasajili sare ya aina yoyote katika mechi itakayowakutanisha na Rayon Sports watafuzu moja kwa moja awamu ya robo fainali ya ubingwa wa taji hilo la CAF.

  • Tags

You can share this post!

KAWI YA JUA: KenGen yasaka ufadhili wa Sh5.7 bilioni

LAMU: KDF yatoa matibabu ya bure kwa wakazi 500

adminleo