• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Mkewe Waititu mashakani kwa kujenga bila leseni

Mkewe Waititu mashakani kwa kujenga bila leseni

NA PETER MBURU

Mkewe gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu alikamatwa na maafisa wa serikali ya kaunti ya Nairobi pamoja na watu wengine 14, wakiwemo wamiliki wa jumba la Jamii Bora Jumatano, kwa kujenga bila vibali vinavyohtajika.

Baada ya kukamatwa, 15 hao walifungiwa katika seli za makao makuu ya serikali ya kaunti ya Nairobi (City hall), kabla ya kufikishwa kortini.

Kwenye mawasiliano ya simu kati ya magavana hao wawili yaliyosambaa mitandaoni, Gavana Sonko alisikika akimhakikishia Gavana Waititu kuwa angehakikisha mkewe ameachiliwa.

Bw Waitiu naye alisikika akimkumbusha Bw Sonko kuhusu urafiki wao na namna wametoka mbali.

“Waliosalia unaweza kumpigia simu ‘mdosi’. Wacha mimi nimwachilie mama (kwa maana ya mkewe Waititu) pekee. Amri zimetoka juu, nitamwachilia mama pekee lakini wengine mpigie ‘mdosi’,” Bw Sonko anasema kwenye rekodi ya sauti.

Kisha Sonko anamrai Bw Waititu kupunguza semi za bila mpango za kupinga shughuli za ubomoaji zinazoendelea sasa, akimkumbusha kuwa mkewe pia atanaswa, kabla ya kuahidi kumpokeza mkewe Waititu vibali anavyohitaji vya majengo yake.

Hata hivyo, mkewe Waititu alijitetea kuwa alikuwa ametuma maombi kupewa vibali husika, japo vikacheleweshwa.

Baadaye, walifikishwa kortini na mkewe Waititu akaachiliwa kwa dhamana ya Sh80, 000 pesa taslimu, kinyume na habari ya mbeleni kutoka kwa mkuu wa mawasiliano katika ofisi ya Bw Sonko Elkana Jacob, kuwa aliachiliwa kwa Sh50, 000.

You can share this post!

Masharti makali kwa wakulima watakaolipwa na NCPB

Wabunge walimeza hongo ndani ya choo, Wamuchomba afichua

adminleo