• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
UFISADI: Raila ajitosa vitani

UFISADI: Raila ajitosa vitani

Na STEPHEN MUTHINI

KINARA wa Upinzani Raila Odinga amejitosa kwa mara ya kwanza kwenye mjadala kuhusu ufisadi Bungeni, na kutaka uchunguzi uanzishwe kuwatambua waliofadhili hongo ili ripoti kuhusu uagizaji sukari itupwe.

Bw Odinga alisema tangu kuibuke madai ya Wabunge kuhongwa Alhamisi wiki jana ili wakatae ripoti kuhusu sukari mbovu, ni wabunge waliopokea hongo hiyo pekee ambao wamekuwa wakikashifiwa.

Kwa maoni yake, mpokeaji na mtoaji hongo wote wana hatia na hivyo, ni lazima aliyetoa pesa hizo ajulikane na kisha akabiliwe na mkono wa sheria.

“Wale waliowahonga wabunge pia yafaa wakabiliwe. Yafaa tuchunguze, tujue ni akina nani hao na kwa nini walienda kuwapelekea wabunge pesa hizo. Ufisadi hutekelezwa na pande mbili,” akasema Bw Odinga mjini Tala, kaunti ya Machakos alipohudhuria mazishi ya Bi Christine Wausi.Marehemu ni shangaziye aliyekuwa seneta wa Machakos Bw Johnson Muthama.

Aliwaeleza waombolezaji kuwa, yeye na Rais Uhuru Kenyatta wamekubaliana kwamba ufisadi ni janga linalohitaji kuangamizwa, na kwa sababu hiyo, hakuna mtu atakayesamehewa akipatikana.

“Hata kama wewe ni ndugu yangu na umekamatwa ukijihusisha na ufisadi, pole. Utabeba msalaba wako kwa sababu hukuiba au kupokea hongo kwa niaba yangu au kabila lako,” akasema.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM alisema, kutakuwa na kongamano la kitaifa mnamo Septemba ambapo washiriki watajadili kwa uwazi uozo wa ufisadi nchini na vipi umeathiri nchi.

“Septemba 10 tunataka tuzungumze kwa uwazi kama wananchi. Ufisadi umepenya katika kila sekta zikiwemo serikali za kaunti, ile ya kitaifa, Bunge na hata Idara ya Mahakama,” akasema.

Jumatano, Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo, Emmanuel Wangwe alisema yeye na wenzake kutoka eneo la Magharibi wamemwandikia Spika Justin Muturi barua wakimtaka kutumia mamlaka yake kuirejesha ripoti ya sukari ili ijadiliwe tena.

“Tumekutana kama Wabunge kutoka mkoa wa zamani wa Magharibi na kukubaliana kumsihi Spika wa Bunge Justin Muturi arejeshe ripoti hiyo. Lengo letu ni kuokoa wakulima wetu wa miwa ambao ndio wanaathirika zaidi na uagizaji sukari ya magendo nchini,” akasema Bw Wangwe ambaye ni Mbunge wa Navakholo kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya Bunge.

Kuliibuka madai kuwa baadhi ya wabunge walihongwa kwa kati ya Sh10,000 na Sh30,000 ili kuangusha ripoti hiyo, madai ambayo yameibua mgawanyiko mkubwa bungeni.

Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula pia wamependekeza serikali ibuni tume maalumu ya kuchunguza na kutanzua sakata hiyo ya sukari.

Mbunge Mwakilishi wa Wajir, Bi Fatuma Gedi alijitetea kuwa pesa alizodaiwa kuwapa wabunge zilikuwa bahasha za kukusanya mchango wa harusi ya mwenzao, Johanna Ng’eno (Emurua-Dikirr) anayefunga ndoa rasmi kesho.

You can share this post!

Wavuvi watatu wahofiwa kuzama baharini

Mafuta ya upako yakosa kumwepushia mhubiri kifungo cha...

adminleo