• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Wafanyakazi wa benki ndio huibia wateja – DCI

Wafanyakazi wa benki ndio huibia wateja – DCI

Na OUMA WANZALA

MKURUGENZI wa Idara ya Upelelezi (DCI) George Kinoti amefichua kuwa wizi unaofanywa kwenye akaunti za wateja wa benki na wale wa huduma za mitandao ya simu hutekelezwa na wafanyakazi wa taasisi hizo.

Akizungumza kwenye hafla katika hoteli ya Radisson Blu jijini Nairobi, Bw Kinoti alisema ipo haja kwa taasisi za kifedha kuwachunguza kwa makini watu kabla ya kuwaajiri, huku akisisitiza kuwa baadhi ya wafanyakazi huwa na rekodi za uhalifu.

Bw Kinoti alionya kuwa iwapo benki na kampuni nyingine zinazohusika na usalama wa pesa za wateja hazitachukua hatua zifaazo, kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza biashara kutokana na wateja kuhofia kuweka pesa na watu wasiojali usalama wa jasho lao.

“Ni wajibu wa kila mwajiri, hasa anayetaka kuajiri mtu katika taasisi inayohusika na kushika pesa, afanye uchunguzi wa kutosha kuhusu mienendo ya mtu huyo. Kwa bahati nzuri kuna maelezo ya kutosha katika idara ya polisi kuwahusu watu,” akasema.

Ufichuzi wake unajiri wakati kukiwa na malalamiko kutoka kwa Wakenya mbalimbali kwamba wamepoteza kiasi kikubwa cha pesa walichokuwa wamehifadhi kwenye simu zao. Kiasi cha pesa kilichopotea bila ya wateja kuwa na habari kinakisiwa kuwa zaidi ya Sh100 milioni.

Hayo pia yanajiri baada ya kutiwa mbaroni Bw Peter Sungu Nyakomitta, ambaye ni meneja wa tawi la Kisii la benki ya Diamond Trust Bank anayeshukiwa kuiba Sh25 milioni kutoka kwa akaunti ya akiba ya mteja. Uhalifu huo uligunduliwa baada ya benki kufanya ujumlishaji wa hesabu za wateja.

Kwenye kisa kingine sawa na hicho, Bw Abel Onyango, afisa wa uhusiano wa Family Bank, anadaiwa kutoa kutoka kwa akaunti ya mteja Sh1.5 milioni kupitia kwa uoanishaji wa kadi za simu.

DCI kupitia mtandao wa Twitter jana ilisema kuwa Bw Onyango na Bw Nyakomitta tayari wamefikisha kortini na kufunguliwa mashtaka kwa makossa hayo.

Wiki jana, washukiwa raia wa China na Wakenya akiwemo mwanafunzi wa Chuo Kikuu humu nchini walishtakiwa katika mahakama ya Milimani kwa makosa ya kutumia ulaghai wa laini za simu kwa lengo la kuiba.

You can share this post!

Mabasi 12 yaungua katika hali ya kutatanisha

Chebukati aanzisha mikakati ya kuleta mageuzi makuu IEBC

adminleo