• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Hatuna deni la Ruto, ODM na ANC waambia wafuasi

Hatuna deni la Ruto, ODM na ANC waambia wafuasi

Na JUSTUS OCHIENG

VYAMA vya ODM na Amani National Congress (ANC) vilisema kwamba havina deni la kisiasa la Naibu wa Rais William Ruto huku vikimtaka kujiepusha na kampeni za 2022.

Vyama hivyo vinavyoongozwa na Bw Raila Odinga na Bw Musalia Mudavadi vilipuuzilia mbali wito wa Bw Ruto kutaka viongozi hao wamlipe deni la kisiasa kwa kumuunga mkono katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Bw Ruto, Jumamosi, wakati wa sherehe ya kumkaribisha nyumbani mbunge wa Lurambi Titus Khamala katika Kaunti ya Kakamega, alisema alimuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais mnamo 2007. Bw Mudavadi alikuwa mwaniaji mwenza wa Bw Odinga kwenye uchaguzi huo uliozua utata na kusababisha machafuko kote nchini.

Bw Ruto alisema aliwasaidia Bw Odinga na Bw Mudavadi kuwa waziri mkuu na naibu waziri mkuu mtawalia wakati wa serikali ya nusu-mkate iliyobuniwa kumaliza ghasia chini ya mpatanishi hayati Kofi Annan.

Bw Ruto aliteuliwa kuwa waziri wa Kilimo.

Hata hivyo, Jumamosi, Naibu wa Rais alisema kwamba hakunufaika na badala yake alipelekwa katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu wa Jinai (ICC) bila Bw Odinga na Bw Mudavadi kumuunga mkono.

Lakini Bw Mudavadi ambaye pia alihudhuria hafla hiyo alisema kuwa hakukuwa na mkataba wa kutaka Bw Ruto kuungwa mkono 2022 wakati wa kampeni za 2007.

“Rais Uhuru Kenyatta na Bw Ruto walinichezea shere waliponihadaa kuwa wangeniunga mkono katika uchaguzi wa 2013 nyumbani kwangu na kisha wakanigeuka,” akasema Bw Mudavadi.

Badala yake kiongozi wa ANC Bw Mudavadi alimtaka Bw Ruto kujiandaa kwa ushindani mkali katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Jana, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema hakukuwa na maafikiano yoyote baina ya Bw Odinga na Bw Ruto.

“Hakukuwa na maafikiano kwamba endapo Bw Odinga angekuwa Waziri Mkuu amuunge Bw Ruto kuwa rais 2022. Wadhifa wa waziri mkuu haukuwepo wakati huo ulibuniwa kwa muda ili kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007,” akasema Bw Sifuna.

“Bw Ruto ajitokeze na kuwauzia Wakenya sera zake badala ya kutumia madai yasiyokuwa na mashiko,” akaongezea.

You can share this post!

Chebukati aanzisha mikakati ya kuleta mageuzi makuu IEBC

Duale aonya Kadhi Mkuu kuhusu Eid-Ul-Adha

adminleo