• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
KURUNZI YA PWANI: Mikakati yawekwa kuimarisha elimu

KURUNZI YA PWANI: Mikakati yawekwa kuimarisha elimu

HAMISI NGOWA na DIANA MUTHEU

VIONGOZI na wadau wa elimu katika eneobunge la Likoni, Kaunti ya Mombasa sasa wanatafuta mbinu zitakazopiga jeki kuimarika kwa matokeo ya mitihani ya kitaifa miongoni mwa wanafunzi wa shule mbalimbali katika eneo hilo.

Mbunge wa eneo hilo, Bi Mishi Mboko anasema tayari amefanya vikao na baadhi ya wasomi na wataalamu wa elimu kujadiliana jinsi watakavyosaidia wanafunzi kuimarisha matokeo yao kwenye mitihani ya kitaifa.

Alisema mojawapo ya mbinu watakayotumia kuboresha viwango vya elimu ni kuanzisha siku ya elimu itakayoadhimishwa kila mwaka kwa kuwatuza wanafunzi bora katika fani mbalimbali.

Alisema tuzo hizo pia zitawaendea walimu ambao masomo wanayofundisha yamepitwa vyema na wanafunzi kwenye mitihani ya daraja tofauti.

Bi Mboko aidha alidokeza kuwa mbinu hiyo itatumika kama kigezo cha kuwapa wanafunzi waliofanya vyema pamoja na walimu wao motisha kwa matokeo mazuri.

“Katika kuadhimisha siku ya elimu, nitahakikisha nawazawadia wanafunzi kwa vitabu, vikombe na zawadi nyingine kemkem ili kila mwanafunzi aweze kuwa na hamu ya kufanya vyema,’’ akasema.

Alisema kando na kuanzisha siku ya elimu, pia anakusudia kuanzisha siku ya wasomi na wanataaluma ambapo wanafunzi watakuwa na fursa ya moja kwa moja ya kutangamana na kujadiliana nao ili kuelezewa ni njia gani wanafaa kuzifuata ili kuendeleza masomo yao.

Alisema yuko na matumani makubwa kwamba kwa kipindi kifupi kijacho, hali ya elimu katika eneo hilo itaanza kubadilika na kufikia viwango vinavyohitajika.

“Wakati umefika kwa shule zetu pia kung’aa kwa kutoa wanafunzi bora katika mitihani ya kitaifa. Lengo langu ni kuona katika kipindi changu cha uongozi hali ya elimu pamoja na matokeo ya mitihani ya kitaifa yanabadilika,’’ akasema.

Alisema ingawa kwa miaka kadhaa eneo hilo limeshuhudia viwango duni vya elimu pamoja na matokeo yasiyoridhisha kwenye mitihani ya kitaifa, hali hiyo sasa inafaa kuzikwa katika kaburi la sahau.

Akizungumza alipokabidhi darasa moja la shule ya msingi ya Maji Safi lililojengwa na pesa za hazina ya NG-CDF hivi majuzi, mbunge huyo anayehudumu katika kipindi chake cha kwanza, alisema mgawo wa bajeti iliyopita ya hazina hiyo ilipiga jeki sekta ya elimu kwa kuitengea kiasi kikubwa cha pesa.

Alisema katika bajeti hiyo, alitenga zaidi ya milioni 36 za basari kwa wanafunzi wa shule za upili pamoja na Vyuo Vikuu na taasisi za kiufundi ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayebakia nyumbani kwa sababu ya kukosa karo.

Kwingineko, viongozi wa Kiislamu wameshutumu vikali tukio ambapo waandishi wawili wa habari walishambuliwa na kukamatwa Alhamisi. Wanahabari hao walikuwa wakiiangazia hoteli moja ambayo imejengwa karibu na ufuo wa bahari kinyume na sheria, eneo la Shanzu kaunti ya Mombasa.

Akizungumza katika ofisi zao katika eneo la Mwembe Tayari, katibu mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini (CIPK), Sheikh Mohamed Khalifa, alisema waliohusika na kitendo hicho wanapaswa kufikishwa mahakamani mara moja na kupewa adhabu kali.

Hii ni baada ya wanahabari wa Nation Media Group (NMG), Karim Rajan na Laban Walloga kushambuliwa, kukamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Bamburi Alhamisi wiki jana.

‘Tumefadhaishwa na kusikitishwa na walinzi katika hoteli ilioko Shanzu waliowashambulia, kuwajeruhi na kuwasumbua maripota wanaofanya kazi na NMG. Kitendo kama hiki si cha kistaarabu na tunataka wahusika wapewe adhabu inayostahiki ili iwe funzo kwa wengine wenye nia kama hiyo,” Sheikh Khalifa alisema.

Sheikh huyo alisema wanahabari wafaa kuheshimiwa na kwamba uhuru wao unaolindwa na katiba haufai kuingiliwa.

‘Rais Uhuru Kenyatta hivi majuzi alitangaza vita dhidi ya ufisadi. Hatutaki kuona ufisadi unatumika kufunika uovu huu uliotendewa maripota hawa. Mashambulizi na kukamatwa kwa waandishi hawa wa habari halikuwa tendo la kistaarabu.Waandishi wa Habari hutujulisha kuhusu matukio ulimwenguni kote. Uhuru wao unapaswa kuheshimiwa,’akasema.

You can share this post!

KURUNZI YA PWANI: Wakazi kupata shule ya kisasa

TAHARIRI: Afisi ya Kadhi Mkuu ipewe heshima yake

adminleo