• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:21 AM
PLANI ‘B’ YA RUTO 2022

PLANI ‘B’ YA RUTO 2022

Na VALENTINE OBARA

MGOGORO wa kisiasa katika Chama cha Jubilee umechochea Naibu Rais William Ruto kuanzisha mikakati mbadala ya kumwezesha kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu 2022.

Na kwa upande mwingine, washirika wa Bw Ruto wameanzisha kampeni ya kutwaa uongozi wa chama hicho kutoka kwa maafisa wa sasa ambao hawakuchaguliwa kukiongoza. Kwa sasa, chama hicho kim mikononi mwa katibu mkuu Raphael Tuju na naibu mwenyekiti David Murathe.

Kwa miezi kadhaa sasa, kumekuwa na mvutano chamani kati ya wandani wa Rais Uhuru Kenyatta na wale wa naibu wake, Ruto wanaodai kuna njama katika Ikulu kumwekea vikwazo asifanikiwe kushinda urais 2022.

Mivutano hiyo imefikia kiwango cha wanasiasa kadhaa wa Rift Valley ambayo ni ngome ya kisiasa ya Bw Ruto kuamua kusajili vyama vipya vya kisiasa, hatua imayoonekana na wachanganuzi wa kisiasa kama mbinu yao kujiandaa kuhama endapo watachezewa shere katika Jubilee uchaguzi utakapowadia.

Seneta wa Kaunti ya Nandi, Bw Samson Cherargei, alinukuliwa kusema hawawezi kufanya kazi na “maadui wao”.

Chama cha United Republican Party kilichosimamiwa na Bw Ruto kilivunjiliwa mbali wakati Muungano wa Jubilee ulipounganisha vyama vyake tanzu vyote kuunda chama kimoja cha Jubilee.

Mpango wa Jubilee kupatanisha mahasimu hao mnamo Julai uligonga mwamba na sasa Naibu Mwenyekiti wa chama, Bw David Murathe, ametangaza mkutano mpya wiki ijayo kwa lengo la kutuliza joto hilo.

Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria, alizua muhemko chamani aliposema chama hicho kinapasa kuandaa uchaguzi ili kisimamiwe na wanasiasa jinsi ilivyo katika vyama vingine vyenye ushawishi mkubwa nchini kama vile ODM, Wiper na Ford Kenya.

“Sisi pekee ndio tuna chama kisicho na nafasi ya wanasiasa. Wakati umefika Chama cha Jubilee kuwa na nafasi ya wanasiasa kukiongoza.

Inahitajika uchaguzi ufanywe chamani,” akasema mbunge huyo ambaye ni mmoja wa wandani wa Bw Ruto kutoka eneo la kati. Kulingana naye, hiyo ndiyo njia pekee itakayoipa Jubilee nguvu za kutosha kutekeleza malengo yake.

Meli ya Jubilee inayoendeshwa na Rais Kenyatta ilizidi kuyumba baada ya rais kuungana na Kiongozi wa Upinzani, Bw Raila Odinga kwa lengo la kutatua changamoto kuu za kitaifa.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa Jubilee, hasa kutoka maeneo ya Bonde la Ufa ambako Bw Ruto ana uungwaji mkono mkubwa, walilalamika kuwa hatua zinazochukuliwa na serikali tangu wakati huo zimenuiwa kuhujumu nafasi yake ya kushinda uchaguzini.

Miongoni mwao ni Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen, ambaye pia ni Kiongozi wa Wengi katika Seneti aliyepinga misimamo ya serikali kuu kuhusu kupiga darubini utajiri wa watumishi wa umma na ufurushaji wa walowezi kutoka Msitu wa Mau, ambazo alidai ni sera zilizolenga kumharibia Bw Ruto nafasi ya ushindi.

Akizungumza Jumapili, Bw Murathe alikosoa wanasiasa wanaodai Rais Kenyatta hana nia ya ‘kurudisha mkono’ kwa Bw Ruto atakapostaafu 2022 akikamilisha muhula wake wa pili uongozini.

“Si lazima rais aamke kila siku kuambia watu wamchague naibu rais 2022. Hakuna wakati hata mmoja ambapo rais amewahi kusema hatamuunga mkono na kumfanyia kampeni naibu rais, kwa hivyo si haki kwa baadhi ya viongozi wetu kugawanya watu katika mirengo ya Uhuru na Ruto,” akasema.

Aliongeza: “Kama wewe ni kiranja wa serikali, kazi yako ni kusaidia utekelezaji wa ajenda za serikali hiyo. Huwezi kuwa unapinga serikali hiyo hiyo. Kama wewe ni kiongozi wa wengi kazi yako ni kuleta umoja wa viongozi na Wabunge wote kumsaidia rais.”

You can share this post!

Mutomo Youth yajinyanyua baada ya kusambaratika

Auawa kwa kulewa divai na kuiba sadaka kanisani

adminleo