• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
Wafungwa wasusia chakula siku ya pili wakidai kuteswa

Wafungwa wasusia chakula siku ya pili wakidai kuteswa

Na STELLA CHERONO

MGOMO wa wafungwa wa gereza la Industrial Area, Nairobi uliingia siku yake ya pili jana ambapo wamekuwa wakisusia chakula wakitaka Kamishna wa Magereza, Isaiah Osugo awatembelee ili asikize malalamishi yao.

Wafungwa hao ambao wako rumande kwa makosa ambayo adhabu yake ni kifo, wanataka afisa msimamizi wa gereza hilo Samuel Ruto, aachishwe kazi, wakidai amekuwa “akiwanyanyasa na kuwatesa”.

“Tangu aletwe katika jela hili Februari mwaka huu, tumekuwa tukidhulumiwa na kupewa huduma duni kila siku, “ mfungwa mmoja akasema.

Hata hivyo, juhudi z a kuwasiliana na Bw Osugo kuhusiana na malalamishi haya hazikufaulu alipokosa kupokea simu na kujibu ujumbe mfupi.

Wafungwa hao waliongeza kuwa afisa wa gereza kwa jina Wilson Tonui amekuwa akiwachapa na kuwaumiza baadhi yao. Wengine wamejeruhiwa na hata kuuawa kutokana na kichapo hicho.

“SP Wilson Tonui alimchapa mwanamume kwa jina John Kibowen ambaye alikuwa akiishi katika jumba nambari L, mbele ya wafungwa wengine. Mwili wake ulibebwa kwa ambulansi na kusafirishwa hadi katika hifadhi ya maiti ya City.”

Kibowen alikuwa amekamatwa na kushtakwa kwa kosa la kuwahadaa watumiaji wa mitandao ya kijamii kwamba yeye ni Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet. Kesi yake ilikuwa ikiendelea kusikizwa kortini.

Kwenye kanda ya sauti iliyotumwa kwa Taifa Leo ikiandamanishwa na video ikiwaonyesha wafungwa wakigoma, mfungwa ambaye hakutambulisha jina lake alidai kuwa kando na Kibowen, wafungwa wengine wamewahi kuchapwa na wanauguza majeraha.

Walimshtumu afisa msimamizi wa gereza wa kuruhusu dhuluma hizo.

You can share this post!

UFISADI: Kashfa mpya ya Sh1.7b yafichuka Wizara ya Michezo

Maskwota kunufaika na ekari 250 za ardhi

adminleo