• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
IPSOS: Wafuasi wa Raila bado hawajamkubali Uhuru

IPSOS: Wafuasi wa Raila bado hawajamkubali Uhuru

Na PETER MBURU

BADO wafuasi wengi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga hawana imani na uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, licha ya viongozi hao wawili kuafikiana takriban miezi mitano iliyopita, utafiti umeonyesha.

Licha ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuzika tofauti zao mnamo Machi na kuanza kushirikiana, utafiti wa kampuni ya Ipsos unasema asilimia kubwa ya wafuasi wa Bw Odinga bado hawajaridhika na uongozi wa sasa.

Kulingana na utafiti huo, wafuasi wengi wa muungano wa Nasa bado wanatilia shaka kujitolea kwa Rais Kenyatta kukabiliana na ufisadi, iwapo atafanikiwa na ikiwa taifa linaelekea mahali pazuri.

Asilimia 47 ya wafuasi wa Nasa wanaamini kuwa Rais Kenyatta hajajitolea kikamilifu kupigana na ufisadi, kinyume na wenzao wa Jubilee ambao asilimia 60 wanaamini amejitolea.

Vilevile, walipoulizwa ni kwa kiwango gani wanadhani Rais atafanikiwa kupigana na ufisadi, asilimia 29 ya wafuasi wa Nasa walisema wana hakika hatafanikiwa, huku asilimia 16 pekee wakisema kwa hakika kuwa atafanikiwa.

Asilimia 66 ya wafuasi wa Nasa aidha wanasema taifa linaelekea mahali pabaya, idadi kubwa kidogo kuliko ya wale wa Jubilee ambao asilimia 53 wanaungama nao kuwa taifa halijachukua mwelekeo mwema.

Kulingana na maeneo, wakazi wa Nairobi waliongoza kwa kusema taifa halielekei mahali pazuri kwa asilimia 69, wakifuatwa na Nyanza na Western kwa asilimia 65, kisha Mashariki na pwani kwa asilimia 60.

Ni wakazi wa kaskazini mashariki mwa nchi pekee ambao wengi wao wanadhani taifa linaelekea pazuri, asilimia 48 wakikiri hivyo na 30 kusema linaelekea pabaya.

Wengi wa waliohojiwa walitoa sababu za kupanda kwa gharama ya maisha, masuala ya uongozi na ufisadi kuwa sababu kuu za kusema kuwa taifa linaelekea pabaya.

  • Tags

You can share this post!

IPSOS: Kibaki na Raila si wafisadi

IPSOS: Wakenya bado huchagua wanasiasa wakijua ni wafisadi

adminleo