21/08/2018

Mapolo wakabana koo wakipigania kisura

Na TOBBIE WEKESA

KANGEMA, MURANG’A

KALAMENI mmoja aliwashangaza wengi eneo hili baada ya kumshambulia rafiki yake akimlaumu kwa kuharibu mipango yake ya kumuoa kipusa aliyekuwa akimchumbia.

Kulingana na mdokezi, makalameni walianza kurushiana cheche za matusi huku kila mmoja akianika siri za mwenzake.

Penyenye zinasema polo alikuwa ameshauriwa na rafiki yake aachane na kipusa huyo amtafutie mwingine.

Inadaiwa polo alifuata ushauri wa rafiki yake. “Baada ya kugundua kuwa polo alikuwa amemtema, kipusa aliamua kumtafuta mchumba mwingine na wakaoana,” alieleza mdokezi wetu.

Inasemekana majuzi, mrembo alipowatembelea wazazi wake, alikutana na polo njiani. Polo alishangaa kumuona jinsi alivyokuwa amebadilika.

Kipusa alikuwa ameng’ara kwelikweli. Polo alimuangalia na kujuta. Alianza kujilaumu kwa nini alifuata ushauri wa rafiki yake na akaamua kuenda kumzomea.

“Wewe ni rafiki wa aina gani? Uliniambia niachane na yule msichana unitafutie mwingine. Hadi wa leo sijampata huyo mwingine uliyeniambia. Bure wewe,” polo alimfoka.

Duru zinaarifu rafiki alimruka polo. “Mimi sikukuambia uachane naye. Nilikuambia utafute mwingine ili uwe na wawili,” jamaa alidai.
Hilo lilimkeketa maini mwenzake.

“Huyo mrembo sasa hivi angekuwa mke wangu. Wewe ni mjinga sana. Kwanza nitamueleza mkeo kuwa unapenda mipango ya kando sana,” polo alimshutumu jamaa.

Wakazi walibaki midomo wazi. Waliamua kutazama sinema ya bure. “Kama bado unamhitaji si uende kwao ukamuoe. Ameng’ara kwa sababu ana mume.

Kutongoza kwenyewe wewe hujui. Na unajidai hapa eti mwanamume,” mwenzake alimjibu. Duru zinasema wawili hao nusura watwangane makonde.

…WAZO BONZO…