17/07/2018

Mwanamume auawa na jeneza la mamake lililomwangukia

Na MASHIRIKA

SULAWESI, INDONESIA

MWANAMUME alifariki alipoangukiwa na jeneza lililokuwa limebeba mwili wa marehemu mamake katika kisiwa cha Sulawesi, Indonesia.

Mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Samen Kondorura mwenye umri wa miaka 40 alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wamebeba mwili huo kuupandisha kwenye ngazi iliyoundwa kwa miti ya mwanzi.

Kwa kawaida katika jamii ya Toroja inayopatikana eneo hilo, marehemu hupandishwa kwa sehemu maalumu ya juu iliyopambwa inayofahamika kama lakkian, kabla mwili ufanyiwe matambiko ya mazishi.

Kamishna Mkuu wa polisi Julianto Sirait aliambia mashirika ya habari kuwa ngazi iliporomoka wanaume hao walipokuwa wakipandisha jeneza.

“Wakati jeneza la mama lilipokuwa likipandishwa kwenye lakkian wakati ngazi iliposonga ghafla kisha ikaporomoka. Jeneza lilianguka likamgonga mwathiriwa,” akasema mkuu huyo wa polisi.

Video ya mkasa huo wa ajabu ilisambazwa mitandaoni na kuonyesha jinsi wanaume hao walivyoanguka mita kadhaa kutoka juu huku waombolezaji wakitamauka.

Wanaume wote walikimbizwa hospitalini lakini kwa bahati mbaya Kondorura akafariki baadaye, kwa mujibu wa ripoti. Ilisemekana mwanamume huyo alizikwa kando ya mamake.

-Imekusanywa na VALENTINE OBARA