20/08/2018

Pasta atisha kushtaki mwenzake kudai anauza pombe

Na OSBORN MANYENGO

KITALE MJINI

Pasta mmoja mjini hapa ametishia kumshtaki mwenzake anayedai amekuwa akimkejeli kwenye mahubiri yake akidai anauza pombe.

Penyenye zinasema pasta huyo alikasirishwa na madai ya mwenzake kwamba kuna wahubiri ambao huuza pombe ilhali wanajifanya watakatifu.

“Alikasirishwa na matamshi ya mwenzake kwamba kuna wanaojiita wachungaji wa kondoo za Mungu huku wakiwa na biashara ya kuuza vileo.

Pasta huyo alishangaa jinsi watu kama hao wanaweza kukomboa vijana na wazee ilhali wanauza pombe,” alisema mdokezi.

Inasemekana kuwa pasta aliyekerwa na matamshi hayo hakuwa katika kanisa hilo lakini baadhi ya waumini walirekodi mahubiri hayo kwa simu na kumpelekea.

Nia ya waumini hao haikujulikana mara moja lakini kasisi aliposikia matamshi hayo alitishia kwenda mahakamani kumshtaki mwenzake akimlaumu kwa kumharibia jina.

Inasemekana kuwa mwana wa pasta aliyekasirika anamiliki duka moja la kuuza pombe kali mjini Kitale na alikuwa akionekana hapo akiongea naye.

“Alikasirika akisema kwamba duka la kuuza pombe sio lake bali ni la mwanawe na hawezi kumkataza kufanya biashara anayopenda kwa sababu ni mtu mzima,” alisema mdokezi.

Inasemekana fununu zilianza kuenea kuwa pasta huyo anamiliki duka la kuuza vinywaji hata kabla ya mwenzake kumkejeli maana walikuwa katika kanisa moja.

Fununu hizo zilifanya pasta na baadhi ya washiriki kuhama kanisa hilo na kuanzisha lake ambapo aliamua kumwanika wazi.

Wazee wa kanisa wamejaribu kuingilia kati ili mambo hayo yasiende kortini lakini inasemekana pasta ameapa lazima amshtaki mwenzake mahakamani liwe liwalo na hatarudi nyuma.

…WAZO BONZO…