16/07/2018

Ruto anavyozimwa asiingie Ikulu 2022

Na BENSON MATHEKA

JUHUDI za kumzuia Naibu Rais William Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta zimechacha huku wanaompiga wakitumia mbinu tofauti ikiwa ni pamoja na kulenga uwezo wake wa kifedha na matamshi yake mwenyewe.

Miongoni mwa matamshi hayo ni aliyotoa Jumapili katika kanisa la All Saints Cathedral kwamba hana deni la kisiasa na jamii au mtu yeyote isipokuwa kutumikia Wakenya.

Wadadisi wanasema japo alilenga kuwazima viongozi wanaosema eneo la Mlima Kenya linafaa kumrudishia mkono kwa kumuunga Rais Kenyatta 2013 na 2017, linaweza kuwa na maana tofauti kuwa Jubilee haitadumu hadi 2022.

Washirika wake wa kisiasa wanasema miongoni mwa mbinu zinazotumiwa kumpiga vita ni kutumia mwafaka wa Rais Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga kuunganisha familia za viongozi wenye ushawishi nchini.

Wadadisi wanasema muafaka huo ulikuwa ni mbinu pana ya kuunganisha familia za viongozi maarufu zenye uwezo wa kifedha kama njia moja ya kumzima Bw Ruto kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 anaolenga kushinda.

Bw Ruto, ambaye anafahamika kama hasla kwa kutoka familia maskini, anasemekana kujiandaa kwa uchaguzi huo lakini wadadisi wanasema familia za Odinga, Kenyatta na Moi zikiungana, zinaweza kumdhalilisha.

Kulingana na mdadisi wa masuala ya kisiasa Godfrey Sang, kuungana kwa familia hizi kumpinga Bw Ruto kunaweza kuwa pigo kwake.

Kwenye maoni katika tovuti ya Star Online, Bw Sang anasema kuna ishara za familia za viongozi maarufu kuungana, japo Bw Odinga na washirika wake wanasisitiza kuwa mwafaka wake na Rais Kenyatta na mkutano wake na Rais Mstaafu Moi haukuhusu siasa za 2022.

Baada ya kutangaza muafaka huo, Bw Odinga alikutana na Rais Mstaafu Daniel Moi, mkutano ambao ulihudhuriwa na seneta wa Baringo, Gideon Moi, anayepigania ubabe wa kisiasa Rift Valley na Bw Ruto.

Kuna ripoti kuwa Bw Odinga amemrai kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi kutoungana na Bw Ruto. Familia ya Mudavadi ina ushawishi wa haja eneo la Magharibi

Profesa Macharia Munene wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU) anasema baadhi ya matatizo ya Bw Ruto ni ya kujitakia.

“Baadhi ya shida za Ruto ni za kujitakia na zingine zimebuniwa dhidi yake. Hiyo ni kawaida katika siasa na kwa kuwa ni mwanasiasa mweledi anajua hayo yote,” anasema Profesa Munene.

Kulingana naye, baadhi ya maadui wa Bw Ruto wanatoka ngome yake. “Ingekuwa ajabu sana kama hangekuwa na maadui kutoka ngome yake na maeneo yote nchini,” alisema.

Wadadisi wanasema wanaopanga kumzima wanatumia umachachari wake katika siasa kulemeza azma yake ya kumrithi Rais Kenyatta 2022.

Miongoni mwa mbinu zao ni kumuacha achape siasa kote nchini. “Unaona, akihudhuria harambee, kunazuka maswali kuhusu pesa zake. Angepunguza ziara zake, angesambaratisha mbinu zao,” asema mbunge mmoja wa Jubilee ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Washirika wa Bw Ruto wamekuwa wakihusisha vita dhidi ya ufisadi na njama za kumlenga Bw Ruto.

Kulingana na Bw Sang, vita hivi vinaweza kulenga kumuangusha Bw Ruto na washirika wake wa kisiasa na kibiashara.

Seneta wa Nandi Kiprotich Cherargei amenukuliwa akisema kuna watu wanaotumia jina la Rais Kenyatta kupanga njama za kumzima Bw Ruto.

Wanaopanga kuzamisha azma yake wanapanga kuzua taharuki ili kusambaratisha chama cha Jubilee, ambacho anapaswa kutumia kugombea urais 2022.

Hata hivyo, Bw Sang anasema itakuwa vigumu kwa Ruto kuacha Jubilee kwa wakati huu.