• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Akina mama na vijana ndio waathiriwa wakuu wa demokrasia ya maelewano – Mzalendo Trust

Akina mama na vijana ndio waathiriwa wakuu wa demokrasia ya maelewano – Mzalendo Trust

NA CHARLES WASONGA

WANAWAKE na Vijana ndio walipoteza zaidi katika demokrasia ya maelewano ilitumika wakati wa uteuzi wa wagombeaji viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Hii ni kulingana na ripoti mpya ya utafiti ambayo imetolewa na shirika la ambalo hufuatilia utendakazi wa asasi ya Bunge nchini Kenya na Afrika, Mzalendo Trust, Februari 18, 2023.

“Ingawa vyama kadha vya kisiasa vilitumia mbinu hii ya demokrasia ya maelewano au muafaka kuamua wale watakaopeperusha bendera zao katika uchaguzi mkuu uliopita, imebainika kuwa mbinu hiyo ilihujumu haki za akina mama na vijana kuwania viti. Mara nyingi udhaifu wao kifedha ndio huchangia kutopendelewa kwao na vyama au miungano ya kisiasa,” akasema Bi Caroline Nyamu, alipowasilisha ripoti hiyo kwa wanahabari katika mkahawa wa Mercure, ulioko mtaa wa Upperhill, Nairobi.

“Katika utafiti wetu tulioufanya baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2022, wanawake na vijana tuliozungumza nao walisema kuwa mbinu hii iliwawekea vikwazo na vizingiti visivyo na maana na kuzima ndoto zao za kuwania vit mbalimbali katika uchaguzi huo,” akaongeza Bi Nyamu, ambaye aliongoza kundi la wataalamu walioendesha utafiti huo.

Demokrasia hiyo ya maelewano huendeshwa kwa njia ya mashauriano na maafikiano, mahojiano ya wapiga kura ili kupata maoni yao au kupitia kura ya maoni ambayo huendeshwa katika eneo mahsusi la uwakilishi.

Japo mbinu  hiyo ya kuamua wagombeaji katika uchaguzi hutumika zaidi katika katika jamii za wafugaji baadhi ya vyama vikuu vya ODM na UDA pia ilitumia mbinu hiyo kama njia ya kuzima ushindani mkali na migawanyika inayosababishwa katika ngome zao.

“Wakuu wa vyama hivi, na vingine, waliohojiwa waliungama mbinu hiyo wakisema unazuia mgawanyiko katika chama, sio ghali na huzima uwezekano wa kutokea kwa ghasia wakati na hata baada ya kura ya mchujo,” Bi Nyamu akawaambia wanahabari alipowasilisha rasmi ripoti hiyo kwa jina “Impact of Negotiated Democracy on Inclusive Politics” (Athari za Demokrasia ya Maelewano kwa Siasa Jumuishi).

Mtafiti wa Mzalendo Trust Bi Caroline Nyamu akiwasilisha ripoti hii kwa jina “Impact of Negotiated on Inclusive Politics” katika mkahawa wa Mercure Hotel-Upperhill, Nairobi. PICHA | CHARLES WASONGA

Hata hivyo, kulingana na Mzalendo Trust mbinu hiyo inahujumu haja ya kuendeshwa kwa uchaguzi kwa njia huru na haki ambapo raia huruhusiwa kuwapigia kura wagombeaji wanaowataka bila kushurutishwa au kuelekezwa.

“Hii ni kwa sababu baadhi ya mikutano hiyo ya kusaka maelewano hufanyika usiku wakati ambapo inakuwa vigumu haswa kwa akina mama kuhudhuria kutoka na majukumu yao ya kinyumbani. Pili, watu ambao huongoza mazungumzo hayo haswa wazee wa kijamii hushawishiwa na fedha ambazo mara nyingi wagombeaji wanaume ndio huwa na uwezo wa kuwapa,” anaeleza Bi Nyamu.

Hii ndio maana Mzalendo Trust inaongeza kuwa wanawake na vijana pia huathiriwa na hali ilivyo sasa ya kutokuwepo kwa sheria ya kudhibiti kiwango cha fedha ambazo wagombeaji viti mbalimbali wanapaswa kutumia wakati wa kampeni.

“Kwa mfano, utafiti wetu uligundua kuwa mgombeaji kiti cha ubunge nchini Kenya anahitaji kutumia kati ya Sh5 milioni na Sh10 milioni wakati wa kampeni. Vijana na akina mama wengi ambao hutaka kuwania viti kama hivi hawawezi kumudu gharama kama hii kwa sababu uwezo wao wa kifedha ni finyu ikilinganishwa na wagombeaji wa kiume,” Bi Nyamu anaeleza.

“Kwa upande mwingine, wagombeaji wa viti vya udiwani (MCA) walitumia angalau Sh5 milioni wakati wa kampeni kiasi cha fedha ambacho vijana na akina mama hawawezi kumudu,” anaongeza.

Kwa upande wake afisa wa mipango wa katika shirika la Mzalendo Trust, Gitungo Wamere, alisema ipo haja kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuweka sheria ya kudhibiti kiasi cha fedha ambazo wawaniaji wa viti mbalimbali wanapaswa kutumia wakati wa kampeni.

“Sheria kama hii ndio itaweka usawa hitaji wakati wa kampeni,” akasema.

Aidha, Bw Wamere alisema kuwa Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa inapaswa kuhakikisha kuwa asilimia 30 ya ufadhili kwa vyama vya kisiasa unatumia kuwapa uwezo wanawake na vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchaguzi.

“Aidha, mashirika ya kijamii yanapaswa kuelekea mahakamani kusaka ufasiri na utafsiri kamili wa demokrasia ya maelewano,” akaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Barcelona wakomoa Cadiz na kufungua mwanya wa alama nane...

Tottenham walaza West Ham United na kuingia ndani ya mduara...

T L