• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Amazon Ladies imani ipo siku itawika katika handiboli

Amazon Ladies imani ipo siku itawika katika handiboli

Na JOHN KIMWERE

NI kweli wahenga hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa walipoketi na kulonga kuwa ‘Lisilokuwapo moyoni pia machoni halipo.’

Ni msemo unaoashiria kwamba hakuna lolote linaloweza kutimia bila ya kufanyiwa kazi. Aidha unafundisha wanadamu kuwa ili kufikia mafanikio yoyote ni lazima wahusika wazamie mpango mzima kuwawezesha kuibuka na mkakati kabambe bila kusahau kujiwekea maazimio yote wanayolenga kufikia.

Katika jukwaa la spoti, msemo huo unahimiza wachezaji nyakati zote kukaza mwendo na kufahamu hadhi wanayolenga kutimiza kufikia kileleni mwa mafanikio yao. Ndivyo wanavyosadiki wachezaji wa timu ya wanawake ya handiboli ya Amazon.

Timu hii ilikuwa miongoni mwa vikosi vilivyoshiriki kampeni za Ligi Kuu nchini muhula uliyokamilika mwezi uliyopita. ”Katika mpango mzima tunalenga kujituma kiume kuhakikisha tunafanya kwenye kampeni za kipute cha msimu ujao nia yetu ikiwa kumaliza kati ya tano bora na kufuzu kushiriki shindano ya Super Cup.”

Timu ya Amazon Ladies…Picha/JOHN KIMWERE

kocha wake Albert Murunga alisema na kuongeza kuwa ana imani tosha wachezaji wake wakizoea watafanya kweli.

AFRIKA MASHARIKI NA KATI

Kocha huyo anashikilia kuwa asiyekubali kushindwa sio mshindani na kutaja kuwa ana mpango kabambe jinsi anavyosaidia kikosi hicho kuhakikisha kimevuruga wapinzani wengine lakini kamwe hawezi kufichua kwa sasa.

Ndio ulikuwa msimu wa kwanza kwa Amazon Ladies kushiriki Ligi Kuu ambapo ilijikuta kwenye wakati mgumu mbele ya wapinzani wakuu Halmashauri ya Nafaka na Mazao nchini (NCPB) na Ulinzi Sharks. Pia malkia wa mchezo huo nchini pia Afrika Mashariki na Kati (ECAHF), Nairobi Water Queens ya kocha, Jack Ochieng.

Amazon iliyojivunia kushinda mchezo mmoja kati ya patashika 14 ilizoshiriki iliibuka ya mwisho nafasi ya nane katika jedwali kwa kuzoa alama mbili.

MAGOLI

Kwenye msimamo huo wenzao waliokuwa karibu ngazi moja ilikuwa Chuo cha Kenyatta (KU) iliyoibuka ya tano kwa alama tisa, moja mbele ya Rangers Ladies. Nao wasomi wa Jomo Kenyatta (JKUAT) walimaliza nafasi ya saba kwa kutia kapuni pointi sita wakijivunia kushinda mechi tatu na kudondosha patashika 13.

Katika jedwali, Nairobi Water Queens chini ya nahodha Gladys Chillo ilihifadhi taji hilo bila kushindwa wala kudondosha alama hata moja ambapo waliibuka kileleni kwa pointi 28. Malkia hao wanaojivunia kushinda taji la ECAHF mara saba mfululizo ndio waliofunga mabao mengi (534) na kufungwa magoli machache (224) msimu uliyopita.

MIAKA IJAYO

Kocha huyo anasema kuwa anadhamiria kunoa makucha ya wachezaji wake ili miaka ijayo baadhi yao wafaulu kuteuliwa kuchezea timu ya taifa. Ingawa kwanza wanalenga kati ya timu bora katika kampeni za Ligi Kuu nchini pia wanatamani kupata nafasi kushiriki mashindano ECAHF.

”Ningependa kushauri wachezaji wote kwa jumla kuwa ili kutimiza malengo yao michezoni wanahitaji kuwa wakizamia mazoezi ili kujiweka fiti.” Kocha huyo anatoa wito kwa shirikisho la Handiboli la Kenya (KHF) kutafuta wadhamini ili kusaidia kwenye shughuli za mechi za ligi nchini.

”Ukosefu wa ufadhili umechangia klabu za Kenya kushindwa kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika isipokuwa Nairobi Water Queens inayojivunia kucheza mara kadhaa,” akasema.

Amazon Ladies inashirikisha wachezaji kama:Lucy Kabura, Nelly Karissa, Rose Atieno, Priscilla Jebet, Elizabeth Wambui, Jacinta Kimani, Faith Atieno, Sylvia Wanjiru, Sarah Gitu, Deborah Nkirote, Jane Omusutsa, Jelry Lelel na Doreen Amojang kati ya wengine.

Timu ya Amazon Ladies…Picha/JOHN KIMWERE

You can share this post!

Gavana Muriithi kusimamia kampeni za Raila

Caroline ajivunia kuwa mwingizaji

T L