• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Apu na teknolojia za kidijitali kuboresha kilimo na ufugaji

Apu na teknolojia za kidijitali kuboresha kilimo na ufugaji

NA SAMMY WAWERU

KENYA ingali mateka ya chakula kinachonunuliwa nje ya nchi, kwa kiwango kikubwa.

Hilo hasa linatokana na wakulima wengi kuendelea kutegemea mifumo ya jadi kuzalisha chakula.

Huku Kenya ikiwa miongoni mwa nchi zilizotajwa na Shirika la Umoja wa Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kuathirika pakubwa na mabadiliko ya tabianchi Upembe wa Afrika, wadau katika sekta ya kilimo; kutoka asasi za umma na kibinafsi, wanakiri umewadia wakati wakulima wabadilishe mifumo ya uzalishaji.

Hatua hiyo aidha inajumuisha ukumbatiaji teknolojia za kidijitali na bunifu za kisasa.

“Kwa sasa, tuko kwenye mizani kubadilisha mifumo na tunahimiza aina yoyote ile ya teknolojia na bunifu kutekelezwa,” Katibu katika Wizara ya Kilimo, Kitengo cha Mimea, Philip Harsama anasema.

Akiainisha manufaa yanayotokana na bunifu za kisasa kuboresha kilimo, afisa huyu anasema Kenya haina budi ila kuenda na nyakati ili kufanikisha oparesheni dhidi ya uhaba wa chakula na njaa.

Samuel Muthui, kutoka Meved Dairy Farm Kirinyaga akielezea kuhusu matumizi ya apu ya kidijitali katika ufugaji. PICHA|SAMMY WAWERU

Sawa na mataifa mengine Barani Afrika, nchi hii ina vipaji tele walio katika umri wa vijana na bunifu zao zikishirikishwa kwenye mtandao wa uzalishaji zitaleta matunda matamu.

Tutajinasua kutoka kwenye minyororo ya njaa na kuepuka kutegemea mataifa ya nje, Katibu anaamini.

“Tunachokosa kama nchi, ni miundomsingi bora na dhabiti kufungua mianya kukuza sekta pana ya kilimo,” Harsama asikitika, akielizea uwepo wa serikali kuafikia ndoto hizo.

Serikali ya Kenya Kwanza, inayoongozwa na Dkt William Ruto ikionekana kupiga jeki sekta ya kilimo, afisa huyu anasema hiyo ni dalili uwepo wake kuiboresha.

Kilimo kinawakilisha zaidi ya asilimia 40 ya nguvukazi nchini, na maeneo ya mashambani asilimia 75.

Samuel Muthui, kutoka Meved Dairy Farm Kirinyaga akielekezwa jinsi ya kupata huduma za kilimo na ufugaji kupitia apu ya kisasa. PICHA|SAMMY WAWERU

Apu za kisasa kutoa huduma, kama vile mafunzo faafu na ya kitaalamu kukuza na kutunza mimea, ni miongoni mwa bunifu zinazohitajika.

Teknolojia hiyo inashirikisha matumizi ya picha, video na hata vipindi kuelekeza mkulima.

Isitoshe, baadhi zina nafasi ya wataalamu kutoa mafunzo ikizingatiwa kuwa kiwango cha idadi ya maafisa wa umma – walioajiriwa na serikali kinazidi kushuka.

“Apu za kisasa zinasaidia kwa kiasi kikuu kutafuta masoko yenye ushindani mkuu,” asema Samuel Muthui, kutoka Meved Dairy Farm Kirinyaga.

Mradi huo wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na pia kuyasindika, kuunda maziwa ya mtindi (yoghurt) ni kati ya washirika wanaonufaika kupitia apu ya Optimerce Consulting Ltd.

Hali kadhalika, wafugaji wanaosambazia kampuni hiyo ya kibinafsi maziwa wanapata huduma, zikiwemo za malipo, kupitia apu ya kidijitali.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge Salasya aanikwa kwa kuruka deni

Mpenzi wangu ataka nitafute mwanamume mwingine maana...

T L