• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Ardhi: Familia 500 zalia kunyanyaswa na matajiri

Ardhi: Familia 500 zalia kunyanyaswa na matajiri

Na MOHAMED AHMED

FAMILIA zaidi ya 500 katika eneo la Bamburi, Mombasa zimelalamikia ubomoaji wa nyumba zao unaodaiwa kutekelezwa na mabwanyenye katika kaunti hiyo.

Familia hizo 527 wa kijiji cha Lamkani, jana zilisema kuwa ubomoaji huo umekuwa ukiendelezwa licha ya maagizo ya baadhi ya tume za serikali kuamuru kuwa ujenzi wowote usiendelezwe kwenye ardhi hiyo ya ekari ya 135.

Mabwanyenye hao wamekuwa wakiendeleza ujenzi wa ua unaozunguka ardhi hiyo yenye utata.

“Tumekuwa tukibomolewa nyumba zetu kwa muda wa wiki mbili mfululizo sasa. Mpaka lini tutaendelea kuishi kwa hofu. Sisi sio wageni katika nchi hii. Sisi ni Wakenya kama wengine na lazima tupate haki ya kuishi kama Mkenya mwengine,” akasema Bi Mwanatumu Mbaruk,90, ambaye ni mmoja wa maskwota hao.

Mwakilishi wa maskwota hao wa Lamkani, Bw Charo Nguma alisema kuwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) ilikuwa imewaelekeza kuwa wafuate serikali kuwapa makao kama inavyostahili.

“Tulifuata mpango huo na vyombo vya serikali na kufikia kwa wizara ya ardhi ambayo ilielekeza kuwa kusifanyike lolote hadi pale uamuzi utatolewa. Lakini cha kusikitisha ni kuwa hilo limepuuzwa na sisi tumeachwa kwenye mateso,” akasema Bw Nguma.

Katika barua kutoka kwa wizara iliyoandikwa mnamo Machi 2019 na Waziri Msaidizi wa Ardhi, Bw Gideon Mung’aro, alielekeza maskwota hao pamoja na familia ya Jonathan Kagiri na wafanyabiashara wanaodai umiliki wa ardhi hiyo, kusuluhisha mzozo huo.

“Mwezi Juni mkutano ulifanyika na kuamulika kuwa kusiwe na ujenzi wowote lakini mabwanyenye hao wamepuuza hilo,” akasema Bw Nguma

Mwanaharakati wa eneo la Pwani , Bi Beatrice Gambo ambaye amehusika katika kusuluhisha mzozo huo alisema kuwa ni vibaya kuona haki za maskwota hao zinakiukwa.

“Ni lazima polisi wajali maslahi ya maskwota hao kwa kuwalinda kwani hiyo ni haki yao kama Wakenya,” akasema Bi Gambo.

Katika barua iliyoandikwa Oktoba 15, 2019, kutoka kwa afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma (ODPP), afisi hiyo ilielekeza maafisa wa polisi kufungua faili ya uchunguzi wa kesi hiyo katika muda wa siku 21.

“Polisi ni lazima wahakikishe kuwa hawapendelei upande wowote ule kwa kutoingilia mpango wa kuleta suluhu kati ya wale wanaozozania ardhi hii,” sehemu ya barua hiyo iliyotiwa sahihi na mwakilishi wa DPP, Bw Devid Fedha ilieleza.

You can share this post!

Aliyechimba kaburi lake mwenyewe ajiua

Kanisa laomba waumini wasisusie uchaguzi wa TZ

adminleo