• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Athari za corona zitawaua Wakenya uchumi usipofunguliwa – Wataalamu

Athari za corona zitawaua Wakenya uchumi usipofunguliwa – Wataalamu

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta anapohutubia taifa leo, anaendelea kusukumwa afungue uchumi ili maskini waache kuteseka kutokana na hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na masharti ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Wengi wanasema masharti yaliyowekwa na serikali hayajafaulu kupunguza maambukizi na vifo.

Wakiongozwa na wakili John Khaminwa, mawakili wanasema iwapo Rais Kenyatta hatafungua uchumi leo, Wakenya wengi watakufa kutokana na athari za kiuchumi kuliko corona.

“Vifo havitaepukika. Serikali haiwezi kuthibiti maisha ya Wakenya 50 milioni. Ni jukumu la kila Mkenya kujikinga binafsi. Ni hali ngumu, vifo haviepukiki na kuporomoka kwa uchumi kutasababisha vifo zaidi,” alisema kwenye taarifa.

Kulingana na Dkt Emmanuel Kiplangat, Rais Kenyatta anafaa kuondoa marufuku ili Wakenya warudi katika shughuli za kawaida za kiuchumi.

“Hali ilivyo kwa sasa ni kuwa maskini wanateseka zaidi kutokana na masharti haya. Tunawaoana wanasiasa, wabunge na magavana wakikiuka masharti haya lakini wananchi wa kawaida wanatakiwa kuyatii wakiambiwa vifo vitaongezeka,” alisema Dkt Kiplangat.

Jana jijini Mombasa, mamia ya wakazi walijazana kwenye fuo za bahari, wakisema wamechoka kufungiwa ndani.

Muungano wa wamiliki wa baa katika kaunti hiyo, unasema huenda hali ikawa mbaya zaidi iwapo Rais Kenyatta ataongeza marufuku.

“Tuko tayari kufuata masharti yote kutoka kwa Wizara ya Afya ili kuhakikisha kuwa wateja wetu wapo salama wanapofika kwenye baa zetu,” akasema Katibu wa muungano huo Kennedy Mumbo.

Lakini baadhi ya viongozi wa kidini na wananchi wanamtaka Rais Kenyatta aendelee kukaa ngumu. Mmoja wao ni Askofu Elvis situma wa Grace Life Ministries mjini Eldoret.

“Kama viongozi wa dini tunaomba makanisa na nchi kwa jumla kufunguliwa lakini nahofia huenda Wakenya wengi wakapuuza maagizo na kuhatarisha maisha,” akasema Askofu Situma.

Mjini Kisumu, mkazi wa Kondele, Bw John Okara, aliunga mkono kauli ya Askofu Situma kwa hofu kuwa watu kutoka Nairobi huenda wakasambaza virusi mashambani.

Ripoti za Benson Matheka, Charles Wasonga, Ahmed Mohamed, Titus Ominde na Tonny Omondi

You can share this post!

Ibrahimovic afunga bao kuisaidia AC Milan kuwapepeta Lazio...

Ruto alia wandani wake kuadhibiwa na Rais

adminleo