• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Baba achezea wagombeaji ODM kwa kutoa tiketi moja kwa moja

Baba achezea wagombeaji ODM kwa kutoa tiketi moja kwa moja

CHARLES WASONGA NA SHABAAN MAKOKHA

HATUA ya chama cha ODM chake mwaniaji urais wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga kutoa tiketi ya moja kwa moja kwa baadhi ya wawaniaji katika kaunti za Kakamega na Kwale kumeibua maswali kuhusu kujitolea kwake kuendesha mchujo wa haki.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama hicho Catherine Mumma wiki jana, chama hicho kitaendesha kura za mchujo kuanzia Ijumaa wiki hii (Aprili 1, 2022) hadi Aprili 21.

Mnamo Jumamosi, Bw Odinga aliwaacha wagombeaji viti vya ugavana na ubunge katika Kaunti ya Kakamega vinywa wazi alipotoa vyeti vya uteuzi kwa baadhi ya wagombeaji wakati wa msururu wa mikutano eneo hilo.

Wabunge Christopher Aseka (Khwisero), Tindi Mwale (Butere), Titus Khamala (Lurambi) na Peter Nabulindo (Matungu) ambao wanaotetea viti vyao walipokezwa vyeti hivyo Jumamosi, Bw Odinga alipozuru maeneo bunge yao.

Wabunge hao waligura chama cha Amani National Congress (ANC) na kujiunga na chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP- K) mnamo Januari mwaka huu baada ya kiongozi wa chama

hicho, Musalia Mudavadi kuungana na Naibu Rais William Ruto kuunda muungano wa Kenya Kwanza.

Lakini kwa mara nyingine wanne hao waligura DAP-K Alhamisi wiki jana na kupokewa na Bw Odinga pamoja na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ka – tika mkahawa wa Serena, Nairobi, ambako ziara ya Kakamega ilipangwa.

Bw Odinga pia alimwidhinisha aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya kusambaza umeme wenye nguvu za juu, Ketroco, Fernandes Barasa kuwa mgombeaji wa kiti cha ugavana wa Kakamega kwa tiketi ya ODM.

“Tuko na Barasa hapa ambaye ni kijana yangu. Yeye ndiye sasa atachukua nafasi ya Oparanya ya ugavana wa Kakamega. Si anatosha?” Bw Odinga akauliza huku wananchi wakijibu “ndio” katika kituo cha kibiashara cha Sabatia, eneobunge la Butere, Kaunti ya Kakamega.

Hatua hiyo ya ODM kupeana tiketi ya moja kwa moja sasa imewaacha kwenye njia panda wawaniaji wengine waliopania kushindana nao katika mchujo baada ya kulipa ada hitajika.

Kwa mfano, katika eneobunge la Butere uteuzi wa Bw Mwale umewaacha Mabw Habil Nanjendo na Achero Mufwayia kwenye baridi licha ya kulipa Sh250,000 kama ada ya uteuzi kwa chama hicho.

Hata hivyo, duru zilieleza Taifa Leo kwamba Bw Nanjendo alihamia chama cha ANC Jumamosi kabla ya mwanya wa kuhama vyama kufungwa saa sita za usiku.

Sasa atawania kiti cha eneobunge la Butere kwa tiketi ya chama hicho kinachoongozwa na Bw Mudavadi, ambaye ni mmoja wa vinara katika muungano wa Kenya Kwanza.

Naye Mbunge wa Shinyalu Justus Kizito ambaye alitaka kushiriki mchujo wa ugavana baada ya kulipa ada ya Sh500,000 alihamia chama cha United Democratic Party (UDP) baada ya Bw Barasa kupewa tiketi ya ODM.

Mbunge huyo ambaye alikuwa mwenyekiti wa ODM katika Kaunti ya Kakamega sasa atawania ugavana kwa tiketi ya chama hicho kinachoongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo.

Katika Kaunti ya Kwale, uamuzi wa ODM kumpa aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Kilimo Profesa Hamadi

Boga tiketi ya moja kwa moja kugombea ugavana umezuia joto huku wafuasi wa wapinzani kutisha kugura chama hicho.

Kiti hicho kilikuwa kimewavutia wagombeaji wengine wanne, akiwemo Naibu Katibu Mkuu Agnes Zani, Spika wa bunge la kaunti ya Kwale Sammy Ruwa na aliyekuwa Mhandisi katika Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA) Chai Lung’anzi.

ODM imetetea hatua yake ya kupeana tiketi ya moja kwa moja kwa wagombeaji hao ikisema hatua hiyo ni halali.

Chama hicho kimesema kuwa ya maoni iliyoendesha ilionyesha kuwa waliopewa vyeti vya uteuzi walikuwa maarufu zaidi kuliko wapinzani wao.

“ODM itatoa tiketi ya moja kwa moja ikiendesha kura ya maoni na kubaini kuwa wawaniaji fulani ndio wenye umaarufu zaidi kuliko wenzao. Mfumo huo ndio ulitumika katika maeneobunge hayo ya Kakamega na Garissa na maeneo mengine,” akasema Bi Mumma.

Katika Kaunti ya Garissa, ODM ilimkataa ombi la Gavana Ali Korane la kutaka kutetea kiti chake kwa tiketi ya chama hicho ikisema tayari imempa mtu mwingine tiketi ya moja kwa moja. Bw Korane saa atarejeshewa Sh500,000 alizolipa kama ada ya uteuzi.

Kulingana na mwenyekiti huyo wa NEB sheria ya uteuzi ya ODM inairuhusu kufanya uteuzi kwa njia ya moja kwa moja, kupitia wajumbe, njia ya mwafaka au ushindani kupitia kura ya mchujo.

Shughuli hiyo itaendeshwa katika kaunti 21 ambako ODM ina ufuasi mkubwa huku ikisaza kaunti 26 zilizoko maeneo ya Mlima Kenya, Ukambani, Bonde la Ufa na Kaskazini Mashariki yanayokisiwa kuwa ngome za vyama tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja.

  • Tags

You can share this post!

Rais Uhuru alainisha baraza la mawaziri bila mbwembwe tele

Rais akabidhiwa fimbo na wazee kuongoza Mlima Kenya

T L