• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Cecafa U23 yaahirishwa kutoka Julai 3 hadi Julai 17

Cecafa U23 yaahirishwa kutoka Julai 3 hadi Julai 17

Na GEOFFREY ANENE

MAKALA ya kwanza ya mashindano ya wanasoka wa Afrika Mashariki na Kati wasiozidi umri wa miaka 23 (CECAFA U23 Challenge Cup) yamesukumwa mbele kwa majuma mawili.

Mkurugenzi wa Cecafa, Auka Gacheo, amesema Juni 28 kuwa kipute hicho, ambacho kilfaa kung’oa nanga Julai 3, sasa kitaanza Julai 17. Mji wa Bahir Dar nchini Ethiopia unasalia mwenyeji wa kombe hilo litakaloruhusu wachezaji watatu waliopitisha umri wa miaka 23.

Gacheo alisema badiliko hilo lilifanywa Juni 28 wakati wa mkutano ulioandaliwa kupitia mtandao wa Zoom na kuleta pamoja makatibu saba kutoka wanachama wa Baraza la Mashirikisho ya Soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Juni 28, Gacheo alisema kuwa badiliko hilo lilisababishwa na baadhi ya mataifa kufungwa kutokana na janga la ugonjwa wa Covid-19 na yanatatizika kupata ruhusa kutoka kwa serikali kuhudhuria mashindano hayo.

Alisema kuwa badiliko hilo pia lilisababishwa na benchi ya kiufundi na baadhi ya wachezaji wa Sudan Kusini kuingia karantini, baada ya kushiriki mashindano ya FIFA Arab Cup mjini Doha, Qatar na wanatarajiwa kurejea nyumbani Julai 7.

Pia, Ligi Kuu ya Tanzania bado haijakamilika hadi Julai 18. Isipokuwa Sudan na Somalia, wanachama wengine wote wa Cecafa wamethibtisha kushiriki. Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ya Under-23 pia itashiriki kama mgeni. Timu ya Kenya inanolewa na Stanley Okumbi.

You can share this post!

Kivumbi na patashika Uingereza ikitifuana leo na Ujerumani...

Shanzu United FC yadondosha alama tatu dhidi ya wenyeji...