• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Chebukati aahirisha uchapishaji wa sajili ya wapigakura baada ya dosari kadhaa kubainika

Chebukati aahirisha uchapishaji wa sajili ya wapigakura baada ya dosari kadhaa kubainika

Na CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) sasa imesogeza siku ya kuchapisha sajili ya mwisho ya wapigakura kutoka Juni 9 hadi Juni 20, 2022 baada ya ukaguzi kubaini dosari nyingi katika sajili hiyo.

Hii ni pamoja na jumla ya wapigakura 246,465 waliokufa, 481,711 waliojisajili zaidi ya mara moja na wengine 226,143 waliojisaliwa kwa kutumia vitambulisho vya kitaifa visivyo vyao.

Ripoti ya awali ya ukaguzi wa sajili hiyo pia imebaini kuwa wapigakura wengine 164,269 walijisajiliwa kwa kwa kutumia vitambulisha na paspoti ambazo sio halali.

Shughuli ya ukaguzi wa sajili hiyo imekuwa ikiendeshwa na kampuni ya ukaguzi ya KPMG tangu Mei 10, 2022.

“Awali, tume hii ilikuwa imetangaza kuwa itaidhinisha na kuchapisha sajili ya mwisho ya wapigakura kabla au mnamo Juni 9, 2022. Hata hivyo, ili kutoa nafasi ya kurekebishwa kwa makosa yaliyobainika wakati wa ukaguzi wa sajili, tume hii imeamua kuchapisha sajili ya mwisho kabla au mnamo Juni 20, 2022,” Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati akasema kwenye kikao na wanahabari katika ukumbi wa Bomas of Kenya mnamo Jumatano jioni.

Alisema kuwa tume hiyo inatarajiwa kupokea ripoti ya mwisho ya ukaguzi wa sajili mnamo Juni 16, 2022 kabla ya kushirikisha wadau kuhusu sajili ya mwisho ya wapiga kura mnamo Juni 17, 2022.

Mkuu wa kitengo cha ushauri katika KPMG Gerald Kasimu alisema walitoa mapendekezo kuhusu sajili hiyo, ambayo yanaweza kutekelezwa mara moja au mengine yanayohitaji muda na uchunguzi zaidi.

“Kuna mapendekezo kadha kwenye ripoti yetu ambayo yanafaa kushughulikiwa kabla ya sajili ya mwishi kuchapishwa na kuwasilishwa kwa IEBC. Baadhi ya mapendekezo hayo yanaweza kushughulikiwa haraka na mengine yatachukua muda kwa sababu uchunguzi unatarajiwa kufanywa kabla ya dosari kusahihishwa,” Bw Kasimu akasema.

Ufichuzi wa dosari hizi katika sajili ya wapiga kura unajiri wiki moja baada ya Naibu Rais William Ruto kuibua malalamishi kwamba karibu wapiga kura milioni moja kutoka ngome zake wameondolewa kutoka sajili ya wapiga kura.

Dkt Ruto ambaye ni mgombea urais kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) chini ya muungano wa Kenya Kwanza, alidai kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kuiba kura kwa manufaa ya wapinzani wake.

“Tuko tayari kufanya kazi na IEBC na marafiki kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu unaendeshwa kwa njia huru na haki. Tunataraji kuwa wahusika wote wakiwemo Umoja wa Ulaya (EU) watapata habari sahihi kutoka kwa IEBC. Tunataka kujua ni kwa nini karibu wapigakura milioni moja waliondolewa kutoka sajili ya wapigakura, na mengi ya majina hayo ni ya watu kutoka ngome yangu,” Bw Ruto akasema.

Alisema hayo alipokutana na ujumbe wa mabalozi kutoka mataifa wanachama wa EU katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi.

Mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga pia ameitaka IEBC kuhakikisha kuwa sajili itakayochapishwa ni sahihi bila dosari yoyote.

Bw Odinga pia ameitaka tume hiyo kuchapisha nakala za sajili hiyo katika afisi zake zote katika wadi, maeneo bunge, kaunti na hatimaye katika makao makuu Nairobi.

“Sajili hiyo pia inafaa kuchapishwa katika tovuti ya IEBC kwa wakati ili wadau wote na Wakenya kwa ujumla waweze kuikagua,” Bw Odinga akasema katika Bomas of Kenya mnamo Juni 5, 2022 alipoidhinishwa rasmi kuwa mgombea urais wa Azimio.

  • Tags

You can share this post!

Mvurya aomba ushirikiano kwa nia ya kuangamiza mihadarati...

Mirema: Dennis Gachoki aachiliwa huru baada ya kukosekana...

T L