• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Chelsea, Arsenal na Man-Utd ni vichapo tu!

Chelsea, Arsenal na Man-Utd ni vichapo tu!

Na MASHIRIKA

EVERTON waliendeleza masaibu ya kocha Mauricio Pochettino kambini mwa Chelsea Jumapili Desemba 10, 2023 kwa kupokeza mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kichapo cha 2-0 ugani Goodison Park.

Mechi hiyo ilikuwa ya saba kwa Chelsea kupoteza katika EPL msimu huu na sasa wanakamata nafasi ya 12 jedwalini kwa alama 19 sawa na Brentford, Wolverhampton Wanderers na Bournemouth waliozaba Manchester United 3-0 ugani Old Trafford, Jumamosi.

Nao mabingwa watetezi Manchester City walisalia katika nafasi ya nne kwa pointi 33 baada ya kutandika limbukeni Luton Town 2-1 ugenini.

Soma pia: https://taifaleo.nation.co.ke/michezo/arsenal-wataruka-kamba-ya-aston-villa-ugani-villa-park

Everton, ambao sasa wameshinda mechi tatu mfululizo ligini kwa mara ya kwanza tangu 2021, ni wa 17 jedwalini kwa alama 13 kutokana na mechi 16. Pengo la pointi nane linawatenganisha na Fulham walioponda West Ham United 5-0 uwanjani Craven Cottage, Jumapili.

Erik ten Hag amesema kichapo ambacho waajiri wake Man-United walipokezwa na Bournemouth “kilimkera” na “kumfadhaisha.”

Aidha, amekiri kuwa kikosi chake “hakiko katika hali nzuri ya kusajili matokeo ya kubashirika miongoni mwa mashabiki” kwa kuwa timu inashuhudia “mwanzo mbaya” ligini.

Kichapo kutoka kwa Bournemouth ndicho cha kudhalilisha zaidi ambacho Man-United wamewahi kupokea chini ya Ten Hag. Naye nahodha Bruno Fernandes amesema matokeo ya sampuli hiyo “hayakubaliki kabisa.”

Baada ya kujikuta chini kufikia dakika ya tano, Man-United hawakutawaliwa na kiu ya kusawazisha. Badala yake, mabingwa hao mara 20 wa EPL walikubali kuangushwa na Bournemouth wiki moja baada ya Newcastle kuwapepeta 1-0 katika EPL ugani St James’ Park.

Hata hivyo, ushindi wa 2-1 waliovuna dhidi ya Chelsea ligini mnamo Desemba 6 ulitarajiwa kuwapa motisha ya kuteremkia Bournemouth.

“Nilitarajia matokeo ya kuridhisha kabisa. Lakini vijana walianza mechi hiyo vibaya na dalili zote zinaashiria kuwa bado hatujafikia ubora wetu,” akasema Ten Hag ambaye sasa anakabiliwa na presha ya kupigwa kalamu kutokana na msururu wa matokeo duni.

Baada ya kualika Bayern Munich ya Ujerumani kwa mechi ya marudiano ya hatua ya makundi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) hapo kesho, Man-United watavaana na Liverpool na West Ham United ugenini kabla ya kualika Aston Villa.

Watafunga kampeni zao za Desemba kwa pambano la EPL dhidi ya Nottingham Forest ugani City Ground.

Man-United sasa wamepoteza jumla ya mechi 11 katika mashindano yote msimu huu, idadi hiyo ikiwa sawa na ya michuano ambayo wameshinda.

Pambano dhidi ya Bournemouth lilikuwa lao la saba kupoteza kutokana na mechi 16 zilizopita ligini.

Sasa wana alama 27, nane nyuma ya nambari tatu Aston Villa waliotandika Arsenal 1-0 ugani Villa Park.

Matokeo ya Villa yaliwawezesha kuendeleza presha kileleni mwa jedwalini na kudhihirisha kuwa wao pia ni wagombezi halisi wa taji la EPL msimu huu. Sasa ni pengo la pointi mbili pekee ndilo linawatenganisha na viongozi wa jedwali, Liverpool.

Ushindi wao ulikuwa wa 15 mfululizo katika EPL nyumbani na ulikomesha fomu nzuri ya Arsenal waliokuwa wameshinda michuano sita mfululizo katika mashindano yote.

Ni mnamo 1980-81 walipotawazwa wafalme wa EPL ambapo Villa walifaulu kujizolea alama nyingi zaidi baada ya mechi 16 za ufunguzi wa msimu wa EPL.

Kikosi hicho sasa kimeshinda mechi nane za kwanza katika EPL ugani Villa Park kwa mara ya kwanza tangu 1932-33.

  • Tags

You can share this post!

Mwanawe Rais wa Somalia atoroka Uturuki baada ya kuua...

Murkomen amshtaki Cherargei vita vya ubabe Bonde la Ufa...

T L