• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Chiloba asema tuhuma dhidi yake ni ‘madai tu’

Chiloba asema tuhuma dhidi yake ni ‘madai tu’

NA CHARLES WASONGA

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (CA) aliyesimamishwa kazi, Ezra Chiloba, amekana tuhuma alizoelekezewa za kuhusika katika sakata ya kifedha katika asasi hiyo na usimamizi mbaya.

Bw Chiloba ametaja tuhuma hizo zilizoko katika ripoti ya ukaguzi wa usimamizi wa fedha katika CA kama madai tu.

“Haya ni madai tu. Nitasubiri mkondo wa haki ufuatwe ili ukweli kuhusu suala hili ujulikane,” akanukuliwa Jumatano akisema kwenye mahojiano mafupi saa chache baada ya bodi ya tume hiyo kumsimamisha kazi kwa wakati usiojulikana.

Mnamo Jumatatu jioni, Bw Chiloba alisimamishwa kazi baada ya mkutano wa bodi ya CA ulioongozwa na mwenyekiti wake, Mary Wambui.

“Baada ya mkutano wa bodi ya Mamlaka hii uliofanyika Septemba 18, 2023, na kupendekeza kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi mkuu, ni furaha yangu kujulisha wafanyakazi kuhusu uteuzi wa Christopher Wambua kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu kuanzia leo (Jumatatu, Septemba 18, 2023,” hadi wakati usiojulikana,” akasema Bi Wambui kwenye taarifa.

Kulingana na ripoti ya ukaguzi, Chiloba alijipendelea kwa kutuma maombi na kuidhinisha mkopo wake wa nyumba kwa kiwango cha juu kwa thuluthi mbili.

Aidha, afisa huyo anadaiwa kujihusisha na mgongano wa kimasilahi kwa kujitwika wajibu wa kuwa mnunuzi na muuzaji katika biashara ambapo CA ililipa Sh25 milioni.

Bw Chiloba pia analaumiwa kwa mienendo mibaya na ukiukaji wa maadili baada ya kubainika kuwa alinunua nyumba na shamba la ukubwa wa ekari saba badala ya shamba la ekari moja inavyohitajika na mpango wa watumishi wa umma kuhusu ununuzi wa nyumba.

“Vile vile, mkurugenzi huyo mkuu aliwasamehe wafanyakazi waliogura CA wakiwa na mkopo wa kima cha Sh28.9 milioni na akapunguza masalio ya mikopo ya wafanyakazi wa zamani,” ikasema ripoti hiyo ya ukaguzi.

Ripoti hiyo pia ilifichua sakata ya usimamizi mbaya wa mpango wa mkopo wa nyumba katika mamlaka ya CA, ambao umetoa mkopo wa zaidi ya Sh662 milioni kwa wafanyakazi wa sasa na wale wa zamani.

Inapendekeza hatua za kinadhamu zichukuliwe dhidi ya Bw Chiloba na maafisa wengine watano wa ngazi za juu katika mamlaka hiyo.

Maafisa hapo ni pamoja na wakurugenzi wa idara za huduma za wafanyakazi, huduma za kisheria, huduma za kifedha na mkaguzi wa ndani.

Ukaguzi huo, ambao uliendeshwa na idara za ukaguzi za CA na Hazina ya Kitaifa, uliamriwa na bodi ya mamlaka hiyo mnamo Mei 2023.

Imefichua kuhusu jinsi wafanyakazi wa sasa na wa zamani wa mamlaka hiyo walivyotumia vibaya mpango huo wa mkopo wa nyumba.

Uovu huo, haswa uliendeshwa kupitia matumizi ya wataalamu wa kibinafsi wa kukadiria thamani ya mali kama nyumba na ardhi waliotoa thamani ya juu.

Kuhusiana na tuhuma za Bw Chiloba, ilibainika kuwa wakadiriaji hao wa kibinafsi waliweka thamani ya nyumba na ardhi ambayo afisa huyo alinunua kuwa Sh25 milioni.

Hii ni licha ya kwamba wakadiriaji wa serikali waliweka thamani ya mali hizo kuwa Sh16.72.

Ripoti hiyo ya ukaguzi inasema kuwa Bw Chiloba aliomba na kuidhinisha mkopo wa nyumba kumwezesha yeye kununua mali hiyo kutoka kwa Simiyu Wakhungu.

Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Uchumi wa Kidijitali Eliud Owalo amesema ofisi yake haihusiki na kutimuliwa kwa Bw Chiloba, akifichua kwamba masuala ya usimamizi na uongozi hushughulikiwa na idara husika.

  • Tags

You can share this post!

Anavyopunguza gharama kufuga kuku kwa kutumia Azolla

DCI kutoka makao makuu wafika Mombasa kuchunguza kifo cha...

T L