• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Hasara baada ya Rwanda kufunga mpaka wake na UG

Hasara baada ya Rwanda kufunga mpaka wake na UG

Na MASHIRIKA

SERIKALI za Uganda na Rwanda ziliendelea kulaumiana kuhusu mzozo uliosababisha mpaka wa nchi hizo mbili kufungwa.

Taharuki ilitanda Jumatano iliyopita wakati magari yote ya mizigo kutoka Uganda yalipokatazwa kuingia Rwanda kupitia mpaka wa Katuna-Gatuna.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Rwanda, Richard Sezibera alisema ingawa “hakuna mtu anakatazwa kusafiri hadi Uganda,” Wanyarwanda wameshauriwa dhidi ya kwenda katika nchi hiyo.

“Wanyarwanda wameshauriwa vikali kutoenda Uganda. Hii ni kwa ajili ya usalama wao wenyewe. Kulikuwa na masuala ya kiusalama kwa waliovuka kuingia Uganda kwa hivyo Wanyarwanda wameshauriwa dhidi ya kwenda nchini humo kiholela, lakini hii haimaanishi wamepigwa marufuku kufanya hivyo,” akasema.

Mnamo Alhamisi, mamia ya wasafiri walikwama katika mpaka wa nchi hizo mbili baada ya maafisa wa uhamiaji kuwazuia kuingia Uganda.

Baadhi yao walisihi maafisa wa mpakani wakieleza mahitaji yao ya kusafiri ni ya dharura lakini hawakusikilizwa. Iliwabidi kurejea Kigali, safari iliyowachukua saa mbili.

Ilipofika Ijumaa, kulikuwa na Wanyarwanda wachache mno Gatuna ambao walikuwa wanatarajia wataruhusiwa kuingia Uganda lakini maafisa walishikilia msimamo wao.

Miongoni mwao kulikuwa na wazee wa kike na wa kiume ambao walitaka kutembelea jamaa zao katika wilaya iliyo karibu ya Kabale.

Gatuna ni mojawapo ya maeneo ya mipakani yenye shughuli nyingi zaidi, likiwa na wasafiri kutoka Uganda, Kenya na hata Sudan Kusini.

Jijini Kampala, Waziri wa Masuala ya Kimaeneo wa Uganda, Philemon Mateke alitaja hatua ya Rwanda ya kuzuia usafirishaji mizigo na watu mpakani kama tangazo la vita vya kibiashara.

“Hatujui wana nia gani lakini tunadhani ni tangazo la vita vya kibiashara,” akasema.

Madereva wa malori waliohojiwa walisema hawakujulishwa kuhusu mpango wa kufunga mpaka huo na hivyo wakapata hasara kubwa.

Biashara ziliathirika pakubwa kwani mizigo haingevukishwa mpakani na pia wafanyabiashara wadogo walikosa mbinu ya kusafirisha mizigo yao.

Hali hii ilitokea wakati ambapo kuna uhasama mkubwa wa kisiasa kati ya Rwanda na Uganda.

Awali kwenye mahojiano na gazeti la The East African, Rais Paul Kagame wa Rwanda alisema uhusiano wa nchi hizo mbili haustawi kwa sababu viongozi hawana nia ya kusuluhisha tofauti zao.

Msemaji wa Serikali ya Uganda, Ofwono Opondo alishangaa kwa nini Rwanda ilifunga mpaka huo bila kutoa sababu yoyote kwani hakuna chuki yoyote dhidi ya Wanyarwanda nchini Uganda.

You can share this post!

OBARA: Serikali iingilie kati mikopo hii ya kidijitali

Miradi iliyokwama yageuka silaha dhidi ya Ruto

adminleo