• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
‘Janga au jambo baya linaweza likaleta fursa nzuri’

‘Janga au jambo baya linaweza likaleta fursa nzuri’

Na MWANGI MUIRURI

PURITY Namalwa Nasilwa, 22, anachukulia janga la Covid-19 kama ‘laana njema’ iliyomwezesha kufumbua macho na kuona fursa ya kujipa riziki baada ya maisha ya dhiki.

Anasema kuwa hili janga lilimng’oa kutoka ajira yake ya kuuza supu na mutura katika vioski vya Mji wa Murang’a lakini katika maisha magumu yaliyomfuata, akalitumia janga lili hili kulipiza kisasi dhidi ya maradhi ya Covid-19.

Ikawa namna gani? Ngoja kwanza.

Mwanadada huyu alikuwa amefanya mtihani wake wa kidato cha nne (KCSE) mwaka wa 2018 na ambapo alipata gredi ya B- na akapata barua ya mwaliko kujiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU).

Kipato cha chini cha familia yao hakikumwezesha kutii mwaliko huo na ndipo aliingia mtaani kusaka kazi.

Kazi aliyopata ni hiyo ya kuuzia watu supu na mutura na pengine akipata badiliko la ajira, akawa yuajipata akiuza uji katika hoteli za mji wa Murang’a,

“Unionapo hivi, nimekuwa na maisha magumu kiasi kwamba nimezoea mambo kuniendea ndivyo sivyo,” asema.

Aongeza: “Lakini katika hali hizo zote, Mungu amekuwa mwema kwangu kwa kuwa amekuwa akinipa ule ujasiri wa kukabiliana na hali na kuwa na uvumilivu wa kuishi siku kwa siku bila kujali makali kwa sababu ya kipato changu duni.”

Katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu ambapo alikuwa akiuza katika vioski na hoteli, mshahara wake ulikuwa kati ya Sh100 na Sh200 kwa siku huku akiwa mpangaji katika nyumba ya Sh2,500 kwa mwezi.

Pato lake kwa ujumla likiwa ni kati ya Sh3,000 na Sh4,000 kwa kuwa hata sio siku zote alikuwa akipata nafasi ya kujipa hilo pato.

Katika ile hali ya kusukumana na maisha akijaribu kujipa afueni ya nyongeza ya hela hapa na pale, huku na kule, akajipata na uja uzito.

Hata wakati Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria alilegeza masharti dhidi ya biashara na kuamrisha hata vioski vya chakula virejelee huduma mwezi wa Mei, “sikupata afueni kwa kuwa biashara zilikuwa zimeishiwa na pesa za kulipa kodi na mishahara ya wafanyakazi wake na ndipo ajira yangu ikakatika ikienda.”

Akiwa na malimbikizi ya kodi ya Sh5,000 na njaa ikimwandama pamoja na mtoto wake mchanga, mkosi wake wa kimaisha alianza kuuona kwa uhalisia wa makali ya kikatili na ambapo ulikuwa hata na uwezo wa kumwangamiza.

Purity Namalwa Nasilwa, 22, akiandaa juisi mjini Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

Asema kuwa hangengojea mauti ndani ya nyumba na ndipo alifanya uamuzi wa kumsaka mamake mzazi mjini Murang’a ili ampe angalau kopo la lolote liokoe hali yake na ile ya mtoto wake.

“Alinipa Sh1,000. Ukarimu huo ulikuwa wa kipekee kwa kuwa hata yeye maisha yalikuwa yanamkalia magumu. Nilijipata katika hali telezi ya kuafikia bajeti ya kutumia usaidizi huo wa mamangu. Nikaamua niingie kwa duka nijinunulie hifadhi ya chakula lakini wazo ndani ya bongo langu likaniuliza jinsi nayo kero ya malimbikizi ya kodi ingeshughulikiwa,” asema.

Alikuwa amesoma katika Biblia kuhusu mbegu ya baraka na ambayo ikipandwa mtu ana uwezo wa kuleta mavuno kemkem kupitia uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kuibariki moja kwa moja.

“Nilichukulia usaidizi huo wa mamangu kama mbegu hiyo inayotajwa katika Biblia ambayo kwa kizungu inafahamika kama The Mustard Seed. Ni lazima ningepata mbinu ya kuipanda maishani na nimtegemee Mungu aibariki inawiri,” asema.

Katika uchambuzi wake wa virusi vya corona na jinsi vilivyokuwa vimehangaisha watu na biashara zao, alipata kuwa kulikuwa na mwanya wa pato ambao ulikuwa unajitokeza ndani ya janga hilo.

“Watu walikuwa wakianza kusaka chakula na vinywaji ambayo huongeza kinga mwilini. Hasa watu walikuwa wakianza kusaka juisi asilia na ndipo nikaanza kuona maisha kwa miwani mingine ya tumaini la maisha ya baadaye,” asema.

Alichukua ile noti ya Sh1,000 na akaingia dukani na kununua chakula cha Sh300.

Purity Nasilwa aonyesha baadhi ya matunda anbayo huuza na pia kuyatumia kutengeneza juisi. Picha/ Mwangi Muiruri

“Nilibaki na Sh700 ambazo nilitumia kununua maparachichi ya Sh40, mananasi ya Sh50, ndizi mbichi za Sh50 na garlic ya Sh100 bila kusahau bitlutes za Sh80, miwa ya Sh50 na nyanya za Sh30. Nilibaki na Sh300 ambazo nilinunua vikombe vya plastiki na jagi kwa ujumla wa Sh200 na nikabaki na Sh100 kwa mfuko,” aeleza.

Aliingia mjini Murang’a na kwa kuwa alikuwa amejulikana na wengi waliokuwa wateja wake wa supu na mutura akaamua kutumia kujulikana huko kusaka usaidizi wa pahala pa kuketi akiuza juisi za matunda hayo asili.

“Wa kwanza niliyemwendea ndiye alikuwa wa kwanza kunisaidia na ambapo alinitengea nafasi kidogo ndani ya biashara yake ya huduma za Intaneti na pia nje ya biashara hiyo akanikubalia niwe nikiweka matunda mengine ili wa kuyanunua anunue akajitengenezee juisi yake nyumbani kwake na wa kununua juisi niliyotengeneza anunue hapo ndani,” asema.

Anasema kuwa aliyaona maajabu ya Mungu na ndipo akang’amua kuwa kwa kweli katika kila hali “Muumba huwa anakushughulikia na ni vile tu wewe katika ubutu wa imani yako huwezi ukafahamu kuhusu hilo.”

Anasema kuwa siku ya kwanza ya biashara yake mpya aliuza juisi ya Sh1,500 na ambapo faida yake ilikuwa Sh700. Siku ya pili hali ikawa vivyo hivyo na baada ya wiki moja, faida ilikuwa imeanza kutinga kiwango cha Sh1,000 kwa siku.

“Kwa sasa, janga la corona kwangu ni laana ya baraka. Sihitaji sasa kusaka kazi na lile kero la kodi limenikoma. Mtoto wangu na pia mimi tuko sawa na nashukuru Mungu kwa kunipa njia katika janga hili ambalo wengi wanaripoti kuhusu kukosa au kupotea njia katika hali za kiriziki,” apiga dua.

Hata hivyo, anasema kuwa tegemeo lake la maisha ni kutumia biashara hii yake kujijenga akitarajia pia kuwa atapata mwanya wa kupata udhamini wa kujiunga na chuo kikuu afuatane na elimu ya kumpa taaluma ndani ya sekta ya chakula na vinywaji.

You can share this post!

Viongozi wa Pwani walalama kuhusu unyakuzi ardhi ya umma

Mama afariki na mwanawe baada ya kukanyaga waya wa umeme...

adminleo