• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Kalonzo amwambia Raila amsahau kura za 2022

Kalonzo amwambia Raila amsahau kura za 2022

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amesema kuwa hawezi tena kuwa mgombea-mwenza wa kiongozi wa ODM Raila Odinga ikiwa atatangaza kuwania urais mnamo 2022.

Kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha Citizen mnamo Jumanne usiku, Bw Musyoka alisema kuwa hawezi kuwa mgombea-mwenza wa mtu mwingine kwenye kinyang’anyiro cha urais, kwani wakati wake wa kuwania nafasi hiyo sasa umefika.

“Naweza kuonekana kama mtu aliyepagawa, ikiwa naweza kuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga kwa mara ya tatu. Safari yangu ya kisiasa haimaanishi kwamba kazi yangu ni kuwa ‘mgombea-mwenza kitaaluma’,” akasema Bw Musyoka.

Kiongozi huyo alisema kuwa atakuwa amekosea pakubwa, kwani amekuwa akipata shinikizo kutoka kwa wafuasi wake kuwania urais kwa sababu wengi wao wanaamini katika uwezo wake wa kisiasa.

Kauli hiyo inajiri huku ikiwa ingali kubainika ikiwa Bw Odinga atawania urais mwaka wa 2022 ama la.

Bw Musyoka alikuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga kwenye chaguzi kuu za 2013 na 2017 ila wakashindwa na Chama cha Jubilee (JP).

Bw Musyoka pia alijitetea vikali kuhusu hatua yake ya kutohudhuria hafla ya kumwapisha Bw Odinga kama “rais wa wananchi” mnamo Januari 30, akidai kwamba Bw Odinga alifahamu kwamba hangehudhuria.

“Ndugu yangu (Odinga) alifahamu kuwa mimi, Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na Seneta Moses Wetang’ula hatungefika katika hafla hiyo. Lengo letu lilikuwa kutafuta njia mbadala ambayo tungeshinikiza uwazi kuhusu uchaguzi bila mafarakano ambayo yangesababisha maafa ya watu,” akasema Bw Musyoka.

Kiongozi huyo alisema kuwa hatua ya Bw Odinga kuapishwa ilitokana na ushauri mbaya kutoka kwa wandani wake wa karibu.

“Bw Odinga alishauriwa vibaya na wandani wake ambao walikosa kuzingatia uhalisia wa athari za hatua hiyo na mustakabali wa nchi, hasa taswira yake katika jamii ya kimataifa,” akasema Bw Musyoka.

Kiongozi huyo alijitetea dhidi ya madai yoyote ya kuwa “msaliti” akisisitiza kwamba tangu kujitosa siasani, amekuwa akizingatia ukweli kama nguzo yake kuu.

Bw Musyoka amekuwa akilaumiwa na baadhi ya waliokuwa wandani wa Bw Odinga kama Miguna Miguna, wakidai kuwa “uoga wake ndio uliopelekea” mipango ya muungano wa NASA kusambaratika.

Baadhi yao walidai kuwa kukaa kwake sana nchini Ujerumani wakati hafla hiyo ilipokuwa ikiendelea kulikuwa kisingizio cha kuikwepa.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa si lazima pawepo ghasia ama maafa kwenye shinikizo zozote za kuitisha mageuzi kwenye mfumo wa uchaguzi nchini.

Wakati huo huo, Bw Musyoka alisema alimsihi Rais Uhuru Kenyatta kumwachilia huru Naibu wa Jaji Mkuu Philemona Mwilu anayekabiliwa na madai ya ufisadi.

Inadaiwa kuwa Jaji Mwilu alijipatia Sh12 milioni kutoka Benki ya Imperial Bank kinyume cha sheria.

“Nilizungumza na Rais Kenyatta na alishtuka kusikia kwamba Jaji Mwilu amekamatwa,” akasema Bw Musyoka.

You can share this post!

Obado akimbizwa hospitalini baada ya kulemewa na maisha ya...

TAHARIRI: Mtaala mpya unahitaji umakinifu

adminleo