• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Kiswahili chasajili matokeo bora KCSE

Kiswahili chasajili matokeo bora KCSE

MARY WANGARI na DIANA MUTHEU

KISWAHILI ni miongoni mwa masomo yaliyoandikisha matokeo bora zaidi katika Mtihani wa Kitaifa wa Elimu ya Sekondari (KCSE) 2019 ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku watahiniwa wa kike wakitia fora zaidi kushinda wenzao wa kiume katika masomo mbalimbali.

Kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha alisema kuwa masomo 16 yaliandikisha matokeo bora zaidi ikilinganishwa na masomo 14 katika KCSE mwaka uliopita.

“Masomo 16 yaliandikisha matokeo bora zaidi ikilinganishwa na masomo 14 mnamo 2018. Matokeo ya masomo 11 yalishuka katika mtihani wa 2019 ikilinanishwa na masomo 12 mnamo 2017,” ilisema taarifa.

Kando na Kiswahili, masomo mengine ambayo wanafunzi waliandikisha matokeo bora kushinda matokeo ya KCSE mwaka 2018 ni pamoja na: Kiingereza, Kemia, Biolojia na Fizikia.

Matokeo ya masomo 11 hata hivyo yalidorora katika mtihani wa KCSE mwaka huu ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2018 huku matokeo ya masomo matatu yakisalia sawa na mwaka uliopita.

“Ningependa hasa kutaja Kiingereza, Kiswahili, Kemia, Biolojia na Fizikia kama baadhi ya masomo muhimu ambapo matokeo yalipanda pakubwa 2019 ikilinganishwa na 2018,” alisema Profesa Magoha.

Kulingana na taarifa hiyo, jumla ya wanafunzi 667,222 walishiriki mtihani wa KCSE mwaka huu ambapo watahiniwa 355, 782 sawa na asilimia 51, walikuwa wavulana huku watahiniwa 341,440 ambayo ni asilimia 48, wakiwa wasichana, hivyo kukaribia usawa katika jinsia.

Kulingana na ripoti hiyo, jumla ya wanafunzi 627 walijitwalia alama A, huku 5,796 wakijizolea alama A-.

Watahiniwa wa kike walibobea zaidi kushinda wenzao wa kiume katika mtihani wa KCSE mwaka huu.

Kiingereza, Kiswahili, Somo la Dini ya Kikristo (CRE), Sayansi Kimu, Sanaa na Ufundim, Kijerumani na Ligha ya Ishara Kenya ni miongoni mwa masomo ambayo watahiniwa wasichana waliwabwaga wenzao wavulana katika mtihani wa KCSE 2019

Aidha, jumla ya kaunti 17 ziliandikisha idadi kubwa zaidi ya watahiniwa wa kike katika KCSE 2019 ikilinganishwa na kaunti 18 mwa ukiopita.

Kaunti hizo ni pamoja na Meru, Vihiga, Kiambu, Elgeyo Marakwet, Nyandarua, Tharaka Nithi, Kisumu, Uasin Gishu, Murang’a, Machakos, Kitui, Taita Taveta, Makueni, Kirinyaga, Kakamega, Kwale, na Nandi.

Katika kaunti ya Mombasa, shangwe na nderemo zilitanda katika shule ya upili ya Memon Academy baada ya Fatima Mohamed, 17 alipata alama ya A, pointi 81 katika KCSE.

Akiwa kitinda mimba katika familia ya watoto wa wanne, Fatima alisema kuwa angependa kusomea udaktari katika chuo kikuu cha Nairobi (UoN).

Fatima alisema bidii, kumcha Mungu na msaada kutoka kwa walimu na wazazi ndio ilipelekea mafanikio yake.

“Napenda masomo ya Kiingereza na Fizikia,” Fatima alisema. Mamake, Maryam Bagha, walimu na wanafunzi wenzake walimpongeza.

“Mwanangu alipata alama 417 katika mtihani wa kitaifa ya shule ya msingi (KCPE) na amekuwa akipenda masomo na kutia bidii tangu kitambo. Yeye ni mtiifu na ana nidhamu,” Bi Bagha alisema.

Mwalimu mkuu katika shule hiyo, Joseph Kamau alisema kuwa shule hiyo ina watoto wawili wenye alama ya A, 11 alama A- na wengi walipata B. Kwa jumla, wanafunzi waliofanya mtihani katika shule hiyo ni 93.

Salame Ali, 18 alipata alama ya A-. Katika mtihani wa KCPE alikuwa na alama 408 .

Abdirahman Hassan ambaye alipata alama ya A- na pointi 80 alisema angependa kusomea uhandisi.

Katika shule ya Abu Hureira, Mohammed Hussein, 18 alipata alama ya B+.

You can share this post!

Serikali Kuu kuzinyima fedha kaunti 34 ambazo hazijalipa...

Magoha sasa kukaza kamba CBC

adminleo