• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
KURGAT: Serikali yalenga kumzima kwa kuwa ‘aliiba mamilioni Urusi’

KURGAT: Serikali yalenga kumzima kwa kuwa ‘aliiba mamilioni Urusi’

Na CHARLES WASONGA

WIZARA ya Mashauri ya Kigeni imeitaka Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutomlipa aliyekuwa kamishna wake, Paul Kurgat, malipo yake ya kuondoka afisini kwa tuhuma kuwa aliiba pesa za umma alipohudumu kama Balozi wa Kenya nchini Urusi.

Dkt Kurgat ni miongoni mwa makamishna watatu waliojiuzulu mnamo Aprili 16, baada ya kutofautia na mwenyekiti Wafula Chebukati.

Wengine ni Bi Consolata Nkatha Maina na Bi Margaret Mwachanya. Dkt Roselyne Akombe alijiuzulu kabla ya Oktoba 26, 2017, kura ya urais iliporudiwa. Alidai tume hiyo haikuwa na uwezo wa kuendesha zoezi hilo kwa sababu ya kuingiliwa na maafisa wakuu serikalini.

Kujiuzulu kwa Kurgat na wenzake kulijiri baada ya wenzao wakiongozwa na Bw Chebukati kuidhinisha kusimamishwa kazi kwa Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba kuhusiana na kashfa ya ununuzi wa vifaa vilivyotumiwa katika uchaguzi mkuu 2017.

Chini ya uongozi wa Chebukati, watatu hao wakasema, “ukumbi wa mkutano wa tume hii umegeuzwa kuwa eneo la kusambaza madai ya uwongo, uwanja wa kueneza uadui na mahala pa kung’ang’ania na kusaka utukufu na sifa.”

Kwenye barua kwa kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Balozi Macharia Kamau anadai kuwa Sh178 milioni zilidaiwa kupotea wakati Dkt Kurgat alipohudumu kama Balozi wa Kenya nchini Urusi.

“Kwa hivyo ni yeye alitia idhini ya matumizi ya pesa hizo,” akasema Kamau alipofika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) Jumatano.

Katibu huyo aliongeza kuwa Sh8.6 milioni zingine zilitumika kwa njia isiyo halali kwa kulipa marupurupu kwa watumishi wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni.

“Wizara inawasilisha suala hili kwa IEBC kama mwajiri na kuiomba kwamba malipo yoyote ambayo Bw Kurgat alifaa kulipwa yasimamishwe hadi pale suala hili litakaposhughulikiwa na kukamilishwa,” ikasema barua ambayo iliandikwa mnamo Mei 2 na Bw LM Waweru kwa niaba ya Katibu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni.

Dkt Kurgat alihudumu kama Balozi wa Kenya nchini Urusi kati ya Agosti 11, 2010 hadi Desemba 21, 2015, kabla ya kuteuliwa kuwa kamishna wa IEBC.

Wiki jana Bw Chebukati aliwaambia wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) kwamba hana uhakika kama watatu hao walijiuzulu au la, na kama wao hupokea mishahara yao au la.

Makamishna wa IEBC, sawa na makamishna wa tume zingine za kikatiba hulipwa mishahara kutoka kwa hazina ya pamoja (Consolidated Fund).

Kulingana na Bw Chebukati, Wizara ya Fedha haijajibu barua zake ambapo alitaka kujua kama makamishna hao bado hupokea mishahara yao au la.

Hata hivyo, aliwaambia makamishna hao kwamba watatu hao bado wanatumia magari ya serikali yenye nambari za usajili za GK. Aidha, alisema bado Dkt Kurgat na wenzake bado wanafurahia huduma za madereva na walinzi.

“Watatu hao bado hawajarejesha mali ya tume kama vile magari na vifaa vinginevyo licha ya wao kudai kujiuzulu,” Bw Chebukati akaambia wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na naibu mwenyekiti Bi Esther Wahome.

 

Ubadhirifu wa fedha

Ukaguzi wa akaunti za ubalozi wa Kenya nchini Urusi kuhusu matumizi ya fedha katika mwaka wa kifedha wa 2015/2016, ulioendeshwa na Mkaguzi Mkuu Edward Ouko, ulifichua visa vya matumizi mabaya ya fedha.

Suala hilo linachunguzwa wakati huu na PAC chini ya uongozi wa Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi.

Katika mwaka huo, maafisa wa ubalozi wa Kenya jijini Moscow, Urusi, walilipwa marupurupu ya kuhudumu ughaibuni chini ya kategori ya A2, ambayo hulipwa maafisa wa ubalozi wa Amerika na mataifa mengine chini ya kategori A1. Maafisa wa mataifa ya Uropa pia hulipwa marupurupu ya chini ya kategori hiyo (A1).

Kwa hivyo, maafisa wa ubalozi wa Urusi walilipwa fedha hizo kinyume na agizo kwenye taarifa ya Novemba 2012 kuhusu malipo ya marupurupu aina hiyo.

Kwa kuwa hitilafu hiyo ya malipo ilitokea wakati Dkt Kurgat alikuwa akisimamia ubalozi huo, kuna uwezekano kwamba pesa hizo zitapatikana ikiwa atapatikana na hatia.

Hata hivyo, Balozi Kurgat alijitenga na tuhuma hizo akisema ukaguzi huo wa matumizi ya fedha akitaja sauala hilo kama “la kihistoria” ambalo lilianza kuchipuza mnamo 2007 na ambalo kufikia sasa lilifaa kuwa limetatuliwa wakati huo.

 

Kujitakasa

“Ukitumia kiwango kama hicho cha fedha, shughuli za ubalozi zitakwama. Wizara inafaa kwanza kusuluhisha makosa yaliyotokea kabla ya mimi kutumwa kule. Ni matumaini yangu kwamba PAC itanialika kujitetea na kutakasa jina langu,” Balozi Kurgat akasema.

Kuhusiana na madai kuwa malipo ya Marupurupu ya Huduma katika Balozi za Kigeni, kuhusiana na Ubalozi wa Urusi yalilipwa kwa kiwango cha juu, Balozi Kurgat alisema viwango vya marupurupu hayo huwekwa na Wizara na kwamba “hauwezi kubadilisha viwango hivyo”.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni inachunguza hitilafu hizo za matumizi ya fedha kabla ya kuwasilisha ripoti yake kwa PAC.

Ujumbe wa maafisa sita umetumwa Urusi kuchunguza suala hilo. Majukumu ya maafisa hao ni pamoja na kuchunguza vitabu vya uhasibu na taarifa za benki za ubalozi huo.

Haijulikani ni kwa nini Wizara hiyo inachunguza suala hilo wakati huu ilhali ilipata habari kuhusu hitilafu hizo za madai ya matumizi mabaya ya pesa za umma mnamo 2016.

You can share this post!

Njogu ateuliwa kuinoa Thika United

Tahadhari kuhusu Ebola

adminleo