• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Levante waduwaza Real Madrid kwa kuichapa 2-1 kwenye mechi ya La Liga

Levante waduwaza Real Madrid kwa kuichapa 2-1 kwenye mechi ya La Liga

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Real Madrid, waliduwazwa na Levante mnamo Jumamosi kwa kichapo cha 2-1 katika uwanja wa Alfredo Di Stefano.

Real wanaonolewa na kocha Zinedine Zidane walisakata sehemu kubwa ya mchuano huo wakiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya beki Eder Militao kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya tisa.

Ingawa hivyo, Real walijipata uongozini kunako dakika ya 13 kupitia kiungo Marco Asensio.

Jose Luis Morales alisawazishia Levante kunako dakika ya 32 kabla ya Roger Marti kupachika wavuni goli la ushindi zikisalia dakika 12 kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha pili kupulizwa. Awali, Marti alikuwa amepoteza mkwaju wa penalti.

Atletico Madrid ambao wamesakata mechi mbili zaidi kuliko Real, wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 47, saba zaidi kuliko masogora wa Zidane. Atletico wamepangiwa kuvaana na Cadiz mnamo Januari 31, 2021.

Zidane alirejea uwanjani kusimamia mechi hiyo ya waajiri wake baada ya kukosa mchuano wa awali uliowashuhudia masogora wake wakipiga Alaves 4-1 baada ya kuugua Covid-19.

Kutokuwepo kwa nahodha Sergio Ramos kulimchochea Zidane kutegemea huduma za Militao na Raphael Varane kwenye safu ya ulinzi.

Militao alikuwa awali ameonyeshwa kadi ya manjano kwa kumchezea visivyo Sergio Leon kabla ya teknolojia ya VAR kubatilisha maamuzi hayo ya refa na Militao kulishwa kadi nyekundu.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Real kupoteza mechi kati ya 10 zilizopita za La Liga. Hata hivyo, wamepoteza mechi tatu kati ya nne zilizopita katika mashindano yote ikiwemo ile iliyowashuhudia wakibanduliwa na Alcoyano kwenye gozi la Copa del Rey.

You can share this post!

Kutimuliwa kwa kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kuna athari...

Leopards, Sharks zapaa ligini huku Sofapaka na wanajeshi wa...