• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Mafuta ghali: Wakenya wakerwa na wabunge kujifanya wanawahurumia

Mafuta ghali: Wakenya wakerwa na wabunge kujifanya wanawahurumia

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wamekasirishwa na hatua ya wabunge kujifanya wanawahurumia kwa hali ngumu ya maisha inayowakabili kufuatia ongezeko la bei za mafuta wakisema ni wao ndio waliwasababishia hali hiyo.

Hii inatokana na kauli za wabunge za kukashifu Mamlaka ya Kudhibiti Biashara za Mafuta na Kawi (EPRA) ya kuongeza bei za mafuta kwa mwezi wa nne mfululizo.

Mnamo Jumapili, EPRA iliongeza bei za petroli, diseli na mafuta taa ziliongezeka kwa Sh7.63, Sh5.75 na Sh5 45 mtawalia.Huu ni mwezi wa nne mfululizo shirika hilo kuongeza bei za mafuta huku Wakenya wakiendelea kukabiliana na athari za janga la corona.

Wenye magari wanatarajiwa kuongeza nauli kwa kipindi cha mwezi mmoja na bei za bidhaa muhimu pia zinatarajiwa kuongezeka kufuatia kupanda kwa gharama ya uchukuzi na uzalishaji.

Wakenya walijibwaga katika mitandao ya kijamii kukataa huruma za wabunge wakisema ni wao waliounga sheria ya kuongeza ushuru wa mafuta.

Katibu mkuu wa chama cha ODM Edwin Sifuna aliyetoa taarifa kudai chama hicho hakitaunga hatua ya kuongezea Wakenya mzigo gharama ya maisha wanaokabiliwa na athari za janga la corona alikashifiwa vikali wengi wakidai anajifanya ilhali chama hicho kiliunga ongezeko la ushuru wa mafuta.

“Tunataka tangazo hilo liondolewe kabla ya bei hizo kuanza kutumiwa,” Bw Sifuna alisema kwenye taarifa muda mfupi baada ya EPRA kutangaza bei mpya Jumapili.Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior alitaka shirika hilo kueleza sababu ya kuongeza bei za mafuta.

“Wakenya wanataka maelezo kuhusu ongezeko la bei za mafuta zinazotangazwa na Mamlaka ya Kawi,” Bw Mutula alisema kwenye Twitter.Hata hivyo, Wakenya waliwachemkia wakiwalaumu kwa kulalamika ilhali walikuwa msitari wa mbele kuunga sheria ya kuongeza ushuru wa ziada wa thamani mwaka wa 2013.

Wengine waliwalaumu kwa kuunga kura ya maamuzi itakayotumiwa pesa nyingi ambazo zinatafutwa kwa kuongeza bei ya bidhaa.Kulingana na mwanaharakati Josphine Kuluo, Wabunge wanaolalamika wanawacheka Wakenya kwa kuwa wamekuwa wakiunga kila hatua ya serikali ya kuumiza Wakenya yakiwemo madeni yanayozidi kuongeka.

“Kwani walitarajia pesa zitatoka wapi na hazivunwi Kama maembe? Waache kuwacheka Wakenya, ni wao waliwatumbukiza katika hali hii,” asema.Kwame Owino wa Taasisi ya Masuala ya Uchumi (IEA) anasema ongezeko la bei za mafuta linalosababisha mfumuko wa gharama ya maisha ni matunda ya bunge isiyojali wananchi wa kawaida.

“Hii inatokea wakati bunge inashindwa kufuatilia mamlaka yaliyokabidhiwa taasisi za kuthibiti (sekta mbalimbali),” asema Bw Owino.

Mwanaharakati Ndung’u Wainaina anasema kwamba wabunge wanaounga mageuzi ya katiba hawafai kulalamika kwa sababu wanajua gharama ya maisha itapanda zaidi.

“Kazeni mishipi. BBI inapendekeza maeneobunge zaidi na nyadhifa zaidi za uongozi. Gharama ya kuendesha serikali bila shaka itakuwa juu,” asema.Alisema ongezeko la bei za mafuta ni mwanzo tu wa masaibu ambayo Wakenya watapitia kufadhili ulafi wa wanasiasa.

You can share this post!

Zawadi ya basi kutoka kwa Ruto yazua utata Mlima Kenya

Korti yakataa kutupa kesi ya mauaji dhidi ya Babu Owino