• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:21 AM
Magonjwa ya kisonono, kaswende yalemea vijana nchini Uingereza

Magonjwa ya kisonono, kaswende yalemea vijana nchini Uingereza

NA BENSON MATHEKA

UINGEREZA mwaka 2022 ilirekodi idadi kubwa ya visa vya ugonjwa wa kisonono na kiwango cha juu zaidi cha kaswende kuwahi kuripotiwa kwa miongo kadhaa huku magonjwa ya zinaa (STIs) yakiongezeka, Shirika la Usalama la Afya la Uingereza lilisema Jumanne.

Kuongezeka kwa magonjwa ya zinaa kulikuwa zaidi kati ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, ambao walichangia sehemu kubwa zaidi.

Kulikuwa na wagonjwa 82,592 wa ugonjwa wa kisonono mwaka 2022, ongezeko la asilimia 50 na idadi kubwa zaidi ya kila mwaka kuripotiwa, kulingana na shirika hilo, linalojulikana kama UKHSA.

Wakati huo huo, maambukizi ya kaswende yaliongezeka hadi 8,692, ongezeko la asilimia 15 tangu 1948, shirika hilo lilibainisha.

Kulingana na shirika hilo, kulikuwa na maambukizi mapya 392,453 ya magonjwa ya zinaa yaliyogunduliwa miongoni mwa wakazi nchini Uingereza mwaka 2022, ongezeko la kila mwaka la karibu robo moja.

Inafuatia kuongezeka kwa visa mnamo 2021, kwani idadi iliongezeka kufuatia janga la Covid-19 ambalo lilileta kushuka kwa magonjwa ya zinaa kwa sababu ya ‘lockdown’ ya muda mrefu mwaka 2020.

“Idadi ya watu waliotembelea daktari, uchunguzi wa afya ya ngono na utambuzi wa magonjwa ya zinaa katika kipindi cha 2020 na 2021 ni ya chini kuliko miaka iliyopita, kwa hivyo mwelekeo wa utambuzi kati ya 2021 na 2022 lazima utafsiriwe katika muktadha huo,” UKHSA ilibaini.

Kisonono kinaongezeka kwa watu wa rika zote, lakini kuenea kwake kulikuwa juu zaidi mwaka 2022 miongoni mwa kundi hilo, shirika hilo lilisema.

Kaswende ya kuambukiza ilikuwa ikiongezeka kati ya mashoga, au watu wa jinsia moja wanaofanya ngono.

Shirika hilo lilisisitiza umuhimu wa watu kufanya ngono salama, likibainisha “kondomu ni ulinzi bora” dhidi ya magonjwa ya zinaa huku likihimiza upimaji wa mara kwa mara.

Hamish Mohammed, mshauri mtaalam wa magonjwa katika UKHSA, alisema: “Magonjwa ya zinaa sio tu usumbufu — yanaweza kuwa na athari kubwa kwa afya yako na ya washirika wowote wa ngono.”

  • Tags

You can share this post!

Jaa la taka lasakama watoto wa Mukuru

Oburu Oginga na Ombaka wataka Orengo na naibu wake...

T L