• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Majeraha kikosini Harambee Stars iliyoshtua Misri

Majeraha kikosini Harambee Stars iliyoshtua Misri

Na JEFF KINYANJUI na JOHN ASHIHUNDU

HUENDA Harambee Stars ikakosa huduma za kipa Patrick Matasi na mshambuliaji matata Ayub Timbe itakapocheza na Togo uwanjani Kasarani kwenye mechi ya kufuzu kwa Kombe la Afrika, Jumatatu.

Matasi aliumia paja wakati Timbe akizidiwa na kiwango cha jeraha lake katika mechi nyingine ya Kundi G dhidi ya Misri, Alhamisi.

Timbe alisafiri hadi Ubelgiji kwa matibabu huku akitarajiwa kuwasili Nairobi leo jioni, ambapo kocha Francis Kimanzi anasubiri ripoti ya daktari kuamua iwapo atampanga kikosini.

“Matasi na Timbe wanaendelea kutibiwa na tutategemea ripoti ya daktari kuhusu hali yao,” Kimanzi alisema Ijumaa huku akimpongeza kipa Ian Otieno wa Posta Rangers aliyechukuwa nafasi ya Matasi kwa kufanya kazi nzuri.

Stars inayotarajiwa kurejea nchini leo, ilionyesha kuwa na njaa ya kurejea haraka katika michuano ya AFCON baada ya kikosi hicho kuvuruga Misri kabla ya kuagana kwa sare ya 1-1 kwenye mechi hiyo iliyochezewa uwanjani Borg El Arab jijini Alexandria, Alhamisi, usiku.

Misri inayoorodheshwa ya 49 duniani, iliashiria kuwa tayari kung’ata Kenya inayoshikilia nafasi ya 108 ulimwenguni punde mechi ilipoanza.

Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu kabla ya vijana wa Kenya wakiongozwa na Michael Olunga kwenye safu ya mbele, Ayub Timbe katika wingi kushoto na Victor Wanyama safu ya kati, kuanza kutatiza wenyeji wao maarufu kama Pharaohs (Firauni).

Mambo yalionekana kutumbukia nyongo kwa Harambee Stars katika dakika ya 42 baada ya masihara ya idara ya ulinzi ya Kenya kuzembea na kutuza Misri bao la kwanza lililofungwa na Mahmoud Kahraba aliyerukia mpira uliomshinda kipa Ian Otieno aliyekuwa ameingia mahali pa majeruhi Matasi.

Hata hivyo, Kenya iliyokuwa imejipata kwenye aibu baada ya kukosa kulipa bili ya hoteli, ilirejea mchezoni katika kipindi cha pili kwa ari ya kipekee, na kukomboa bao hilo pale Cliff Nyakeya alipompokonya kwa ustadi mchezaji wa Misri mpira katika eneo hatari na kumpokeza Michael Olunga ambaye hakusita kulipua nduki ndani katika dakika ya 67.

Timbe asumbua ngome ya Misri

Timbe aliyekuwa katika kiwango kizuri kabla ya kutolewa kutokana na jeraha alisumbua ngome ya Misri mara kwa mara lakini juhudi zake za kufunga bao hazikufua dafu.

Nafasi yake ilichukuliwa na Nyakeya ambaye pia alionyesha mchezo wa hali ya juu, huku akikaribi kufunga bao kutokana na mpira wa fri-kiki, nje kidogo ya kijisanduku cha eneo la hatari.

Misri walikaribia kufunga bao la pili dakika ya 81, lakini hatari hiyo ilizuiliwa na walinzi wa Stars wakiongozwa na Joash Onyango.

Mashabiki watalipa Sh200 na Sh500 kushuhudia mechi kati ya Harambee Stars na Togo.

  • Tags

You can share this post!

Ronaldo aiweka Ureno pazuri Euro

Mwanafunzi apatikana amefariki katika chuo kikuu cha Moi

adminleo