• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Man-United guu moja ndani ya fainali ya Carabao Cup baada ya kukomoa Nottingham Forest 3-0 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ugenini

Man-United guu moja ndani ya fainali ya Carabao Cup baada ya kukomoa Nottingham Forest 3-0 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ugenini

Na MASHIRIKA

MARCUS Rashford aliendeleza makali yake msimu huu kwa kufunga bao na kuchochea waajiri wake Manchester United kunusia fainali ya Carabao Cup baada ya kukomoa Nottingham Forest 3-0 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali mnamo Jumatano usiku ugani City Ground.

Rashford aliwaweka Man-United kifua mbele katika dakika ya sita kabla ya mabao mengine kujazwa wavuni na Wout Weghorst na Bruno Fernandes. Ushindi huo mnono unapunguzia masogora wa kocha Erik ten Hag presha kadri wanavyojiandaa kwa pambano la marudiano siku sita zijazo ugani Old Trafford.

Man-United wanapigiwa upatu wa kulaza Newcastle United au Southampton na kutawazwa mabingwa wa Carabao Cup – taji litakalokomesha ukame wa makombe kabatini mwao tangu 2017.

Bao la Rashford dhidi ya Forest lilimwezesha kufikisha jumla ya magoli 10 kutokana na mechi 10 ambazo ametandazia waajiri wake Man-United tangu kukamilika kwa fainali za Kombe la Dunia mwishoni mwa 2022 nchini Qatar.

Aidha, bao hilo lilikuwa lake la tano kwenye kipute cha Carabao Cup na sasa anaselelea kileleni mwa orodha ya wafungaji bora wa kivumbi hicho msimu huu. Goli la Weghorst lilikuwa lake la kwanza tangu ajiunge na Man-United mwanzoni mwa Januari 2023.

Forest waliwahi kutinga fainali ya Carabao Cup mnamo 1992 wakinolewa na kocha Brian Clough. Man-United iliyokuwa chini ya mkufunzi Jose Mourinho ilitandika Southampton 3-2 katika fainali ya Carabao Cup mnamo Februari 2017.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Barcelona wacharaza Real Sociedad 1-0 na kuingia...

Kolera yaua watatu Bura

T L