• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Michenza kitega uchumi tosha kwa mwalimu mstaafu

Michenza kitega uchumi tosha kwa mwalimu mstaafu

NA PETER CHANGTOEK

MATUNDA yenye rangi njano na mengine yenye rangi ya kijani kibichi yananing’inia kwa mimea katika shamba moja lililoko katika eneo la Nziu, katika Kaunti ya Makueni.

Hili ni shamba linalomilikiwa na Peter Mwaka, ambaye alijitosa katika zaraa hiyo takriban miaka 45 iliyopita.

Shamba hilo linajulikana kama Joyland Farms. Mwaka, mwenye umri wa miaka 71, alijitosa katika ukuzaji wa michenza, ambayo hulinganishwa na dhahabu katika eneo hilo.

“Ina faida ikilinganishwa na ukuzaji wa mahindi na maharagwe,” asema mkulima huyo.“Nilianza kwa kuikuza michenza michache, na kuanzia hapo, nikaanza kujikuzia miche yangu na kuongeza mimea polepole,” afichua Mwaka.

Kwa wakati huu, mkulima huyo, ambaye alijitosa katika ukuzaji wa michenza mwaka 1976, hulitumia shamba ekari 36 kuzalisha machenza na machungwa.

Mkulima huyo anasema kuwa, alinunua miche kumi kutoka Afrika Kusini, na kuatika na miche ya milimau. Kila mche ulimgharimu Sh500.

“Nilipoenda Afrika Kusini, nikapata aina hiyo ya miche na nikaja kuipanda nchini Kenya,” aongeza.Kabla hajaipanda miche ya michenza, yeye huhakikisha kuwa shamba linalimwa vizuri.

“Hulima shamba ili kuhakikisha kwamba magugu yanaondolewa. Hunyunyizia dawa pia ili kuzuia na kuondoa magonjwa,” asema Mwaka, ambaye alijiuzulu 2010 kutoka kwa kazi ya ualimu.

Aidha, mkulima huyo hunyunyizia maji kukiwa na kiangazi. Mbali na kufanya hivyo, mkulima huyo anafichua kuwa, hutumia mbolea asilia kwa mimea kila baada ya misimu miwili.

Mkulima huyo anasema kwamba ana maji ya kisima, na sehemu nyingine ya shamba lake hutegemea maji ya mvua.Hata hivyo, anasema kuwa, janga la Covid-19 limeathiri shughuli zake za kilimo kwa njia fulani.

“Kuhitajika kwa matunda hayo hakujawa sawa na bei imekuwa ikipanda na kushuka,” asema, akiongeza kuwa pembejeo za kilimo pia, ni ghali.Mwaka anasema kuwa, wakati anapoipanda miche ya michenza, huchimba mashimo yenye kina cha futi 2 kwa futi 2 kwa urefu, na futi 2 kwa upana.

“Kisha changanya udongo wa juu na mbolea asilia kilo 2, na uupande mche katikati ya shimo,” aeleza, akiongeza kuwa, mchenza huchukua muda wa miaka 2-3 kuanza kuzaa matunda.

Mkulima huyo anafichua kwamba, baada ya muda wa miaka mitano, mmea utakuwa ukizaa matunda kwa wingi.

Anafichua kuwa, wao hukuza michungwa, lakini michenza ndiyo imekuwa ikiwapa faida tele kwa sababu waja wengi huyapenda matunda hayo mno.

Miongoni mwa changamoto ambazo alizipitia hapo awali ni ukosefu wa maji ya kutumia, kabla hajachimba kisima ambacho kwa sasa humpa maji.

“Changamoto nyingine katika kilimo hichI, ni wadudu waharibifu na magonjwa ambayo yasipozuiwa, huathiri mimea na matunda,” anaeleza.

Mkulima huyo anafichua kwamba, huyauza machenza yake kwa bei ya Sh100-Sh200 kwa kilo, hilo likitegemea uchache au wingi wa matunda sokoni.

Mnamo mwaka 2016-2018, Mwaka aliyauza matunda yake katika makao makuu ya dukakuu la Naivas, jijini Nairobi, ambapo alitia kibindoni hela nyingi.

Anadokeza kuwa, amekuwa akitangaza biashara hiyo ya matunda kupitia kwa mitandao ya kijamii na kuna wateja ambao wamekuwa wakishirikiana nao kwa muda mrefu, katika shughuli ya uuzaji wa matunda yenyewe.

“Zaraa ya ukuzaji wa michenza ni nzuri, na haina kazi nzito au kubwa. Ina faida, endapo mkulima ataitunza mimea yake vyema.”

Pia anafichua kuwa, ana mipango ya kuanza kuyauza matunda hayo ughaibuni, miaka miwili kuanzia sasa. Mwaka anasema kwamba, kwa msimu mmoja, hupata matunda tani 70 hadi tani 100.

  • Tags

You can share this post!

Hofu yazuka kuhusu unga kupanda bei

Anapenda upishi, sasa ana kiwanda cha kupika pilipili

T L