• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
‘Morocco ina uwezo wa kutwaa Kombe la Dunia’

‘Morocco ina uwezo wa kutwaa Kombe la Dunia’

NA JOHN ASHIHUNDU

BAADA ya kuandikisha historia kama nchi ya kwanza ya Afrika kutinga nusu-fainali ya Kombe la Dunia, mashabiki wengi wa soka wameanza kuamini kwamba timu ya Morocco ina uwezo mkubwa wa kutwaa ubingwa wa Dunia.

Morocco ilimaliza ya kwanza katika Kundi F baada ya kuandisha matokeo ya 0-0, 2-0 na 2-1 dhidi ya Croatia, Ubelgiji na Canada mtawalia.

Baadaye waliangusha Uhispania kupitia kwa mikwaju ya penaltii katika awamu ya 16 na kufuzu kwa robo-fainali ambapo waliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Ureno na kutinga nusu-fainali, ambapo watakabiliana na Ufaransa Jumatano kuwania nafasi ya kucheza fainali.

Ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Ubelgiji kwenye mechi iliyochezewa Education City mjini Doha mbele ya zaidi ya mashabiki 44,000 ulidhihirisha wasi kwamba kikosi hicho kiko imara kukabiliana na upinzani wowote mbele yake, baada ya mafanikio haya makubwa kuwahi kushuhudiwa Afrika.

Mbali na nchini kwao ambapo mashabiki walimwagika kwa wingi katika mitaa ya miji mikubwa ya Casablanca, Rabat na Marrakesh, mashabiki waliufurahia ushindi huo katika mataifa mengine hasa barani Afrika, Kenya ikiwemo.

Kikosi cha sasa cha Morooco chini ya kocha Walid Regragui ambaye ni miongoni mwa makocha wa kikundi cha kwanza kupata Diploma juu zaidi barani Afrika, huenda kikatimiza ndoto ya mkongwe Pele kwamba siku moja timu kutoka bara Afrika itashinda Kombe la Dunia.

Tangu Pele atoe ubashiri wake miaka ya 1970, kiwango cha juu zaidi timu za Afrika kufika ilikuwa hatua ya robo-fainali ambapo Cameroon ilifanya hivyo mnamo 1990 fainali hizo zilipofanyika nchini Italia, Senegal ikafuata mwaka 2002 (Japan na Korea Kusini) kabla ya Ghana mnamo 2010 zilipofanyika nchini Afrika Kusini.

Itakumbukwa kwamba tangu mashindano haya yaandaliwe kwa mara ya kwanza mnamo 1930 hadi 1962, ni Misri pekee iliyowakilisha bara Afrika mnamo 1934, kwa sababu FIFA ilikuwa imekataa kuipa Afrika nafasi.

Lakini matokeo mazuri ya Algeria, Morocco na Cameroon dhidi ya timu kubwa za Ujerumani Magharibi, Ureno na Argentina miongo mitatu iliyopita ulishtua shirikisho hilo la kimataifa, hadi frika ikapewa nafasi rasmi ya kushiriki.

Kufikia 1982, ni mataifa mawili tu ya Afrika yaliyokubaliwa, halafu nafasi tatu mwaka 1994 na baadaye nafasi tano mwaka wa 1998, baada ya Cameroon kutinga robo-fainali mnamo 1990.

Afrika imekuwa na matokeo duni katika mashindano haya, lakini lazima pia ikumbukwe kwamba yote yanatokana na sababu kwamba bara hilo limewakilishwa mara chache.

You can share this post!

Amerika yapongeza idara ya mahakama Kenya kwa kutoa maamuzi...

Qatar kupata faida ya Sh1.1 trilioni kwa uandalizi wa Kombe...

T L