• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
MOTO BALAA: Griezmann afunga mawili katika ushindi wa Barcelona dhidi ya Real Betis

MOTO BALAA: Griezmann afunga mawili katika ushindi wa Barcelona dhidi ya Real Betis

Na MASHIRIKA

BARCELONA, UHISPANIA

ANTOINE Griezmann alifungua rasmi akaunti yake ya mabao kambini mwa Barcelona kwa kupachika wavuni magoli mawili katika ushindi wa 5-2 uliosajiliwa na waajiri wake dhidi ya Real Betis katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumapili.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Griezmann kutandaza mbele ya mashabiki wao wa nyumbani ugani Camp Nou tangu abanduke kambini mwa Atletico Madrid mwishoni mwa msimu uliopita.

Griezmann ambaye ni mzaliwa wa Ufaransa, aliufanya rasmi uhamisho wake hadi Barcelona kwa kiasi cha Sh14 bilioni kinyume na matamanio ya Atletico wanaonolewa na kocha Diego Simeone.

Carles Perez aliwafungia Barcelona bao la tatu na kuwapa hamasa zaidi kadri walivyopania kujinyanyua baada ya chombo chao kuzamishwa na Athletic Bilbao wiki moja iliyopita.

Jordi Alba na Arturo Vidal ni wachezaji wengine waliowafungia Barcelona kabla ya Lorenzo Garcia kuwapachikia Betis bao la pili.

Betis ndio waliokuwa wa kwanza kuliona lango la Barcelona kupitia kwa kiungo Nabil Fekir mwanzoni mwa kipindi cha kwanza.

Griezmann alikuwa na presha ya kuwaongoza Barcelona ipasavyo baada ya kuonyesha matokeo duni alipowajibishwa kwa mara ya kwanza dhidi ya Bilbao ugenini.

Ulazima wa kutia fora katika mchuano uliowakutanisha na Betis ulizidishwa na tukio la kutokuwepo kwa mafowadi Lionel Messi, Luis Suarez na Ousmane Dembele wanaouguza majeraha.

Barcelona bado wanahusishwa na uwezekano wa kujinasia huduma za mshambuliaji wao wa zamani, Neymar Jr ambaye bado hajachezeshwa na waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) kutokana na suitafahamu inayozingira mustakabali wake uwanjani Parc des Princes, Ufaransa.

Awali, Griezmann alitabika sana kuoanisha pasi zake na za wachezaji wenzake na bao la Fekir kunako dakika ya 15 lilionekana kuwaweka Barcelona katika hatari ya kufungua kampeni zao za La Liga kwa kupoteza jumla ya michuano miwili mfululizo.

Ingawa hivyo, hofu hiyo ilianza kufifia baada ya Griezmann kushirikiana vyema na Sergi Roberto, Nelson Semedo, Sergio Busquets na Arturo Vidal katika mchuano huo uliowashuhudia wakimwajibisha chipukizi wa Guinea-Bissau Ansu Fati, 16, kwa mara ya kwanza.

Mwanzoni mwa msimu huu, Griezmann aliahidi kujituma vilivyo ndani ya jezi za Barcelona hadi atapotia kapuni ufalme wa Mchezaji Bora duniani. Isitoshe, alifichua kwamba kubwa zaidi katika mipango yake ya sasa ni kubadilisha mtindo wake wa uchezaji ili uwiane na ule wa Barcelona.

Akivalia jezi za Atletico waliomsajili kutoka Real Sociedad mnamo 2014, Griezmann alifaulu kupachika wavuni mabao 133 kutokana na jumla ya mechi 257.

Licha ya kuhusishwa pakubwa na uwezekano wa kujiunga na Barcelona au Manchester United yapata mwaka mmoja uliopita, alihiari kutia saini mkataba mpya uliotarajiwa kurefusha muda wa kuhudumu kwake kambini mwa Atletico kwa kipindi cha miaka mitano zaidi kuanzia Juni 2018.

Ingawa hivyo, alifichua azma ya kuagana na Atletico mnamo Mei mwaka huu na akawataka miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kumwachilia kutua ugani Camp Nou kuvalia jezi za Barcelona.

Ujio wake kambini mwa Barcelona unakifanya kikosi hicho kuwa miongoni mwa klabu zinazojivunia huduma za wavamizi mahiri zaidi katika ulingo wa soka.

Uwezo wa Griezmann wa kutamba na mpira katika safu yoyote ya ushambuliaji unatazamiwa kumweka kocha Ernesto Valverde katika nafasi ya kumwajibisha kwa pamoja na Luis Suarez na Lionel Messi katika nyingi za mechi zijazo za Barcelona.

Kunyakua

Akizungumza baada ya mechi dhidi ya Betis, Valverde alikiri kwamba kusajiliwa kwa Griezmann ni zao la hamasa tele ya Barcelona kutaka kunyanyua ubingwa wa soka ya bara Ulaya (UEFA) hasa baada ya kubanduliwa na Liverpool kisha Roma kwenye hatua ya nusu-fainali katika kipindi cha misimu miwili iliyopita.

Katika kipindi cha misimu mitano kambini mwa Atletico, Griezmann alidhihirisha ukubwa wa uwezo alionao uwanjani huku akitegemewa sana kufunga na kuchangia mengi ya mabao.

Huenda fowadi huyu akawa mchezaji wa pili aliye ghali zaidi kuwahi kusajiliwa na Barcelona iwapo miamba hao wa Uhispania watajitwalia upya huduma za mvamizi Neymar Jr kutoka PSG.

Tamanio kubwa zaidi la Neymar kwa sasa ni kurejea upya uwanjani Camp Nou na kufufua ushirikiano wake na Messi kisha Suarez katika safu ya mbele ya Barcelona.

Ingawa hivyo, kurejea kwake Camp Nou kutategemea ukubwa wa ushawishi wa Barcelona dhidi ya Real ambao pia wanaziwania huduma zake.

Kinachowachochea zaidi Barcelona kumrejesha Neymar ni wepesi wa chipukizi wao Ousmane Dembele kupata majeraha mabaya ya mara kwa mara.

Hili huenda likawashawishi waajiri wake kumtupa mnadani hivi karibuni.

Japo Josep Maria ambaye ni Rais wa Barcelona amesisitiza kwamba Dembele ni bora zaidi kuliko Neymar, muhimu zaidi ni kwamba ujio wa Griezmann utafupisha zaidi kipindi cha kuhudumu kwa Suarez uwanjani Camp Nou.

Kwa kuwa Messi na Suarez wote wana umri wa miaka 32, kujishughulisha kwa Barcelona sokoni ni ishara kwamba kikosi hicho kinajiandaa kwa maisha ya usoni bila ya huduma za wawili hao ambao kwa kipindi kirefu, wamekuwa tegemeo kubwa katika safu ya mbele tangu 2014.

Katika muhula mfupi uliopita wa uhamisho wa wachezaji, Barcelona walijivunia huduma za kiungo chipukizi Frenkie de Jong kutoka Ajax ya Uholanzi na Junior Firpo wa Betis.

You can share this post!

UFISADI: Uhuru azimia marafiki simu

Eriksen pua na mdomo kuyoyomea Real

adminleo