• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Msaada hatimaye wawasili Lamu kunusuru wakazi wanaozongwa na mafuriko

Msaada hatimaye wawasili Lamu kunusuru wakazi wanaozongwa na mafuriko

NA KALUME KAZUNGU

WAATHIRIWA wa mafuriko, Lamu wamefikiwa na kupokezwa msaada wa chakula, dawa na vyandarua kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Lamu na wahisani.

Jumla ya familia 369, nyingi zikiwa ni kutoka tarafa ya Witu, Lamu Magharibi, wameathiriwa na mafuriko hayo, ikiwemo nyumba zao kusombwa na kuziacha familia hizo kwenye kibaridi kikali.

Miongoni mwa vijiji vinavyoshuhudia athari kali ya mafuriko Lamu ni Pangani, Marafa, Kona Mbaya, Lumshi A na B, Chalaluma, Pandanguo, Moa na viunga vyake.

Akizungumza mwishoni mwa juma wakati alipoongoza kikosi cha serikali ya kaunti na wahisani, ikiwemo Shirika la Msalaba Mwekundu na wakfu wa Al-Khair, Gavana wa Lamu, Issa Timamy alisema utawala wake utahakikisha kila familia iliyoathiriwa na mafuriko inapata usaidizi.

Bw Timamy aliwashauri wakazi wanaoishi sehemu za nyanda za chini na ambazo zinatambulika kwa mafuriko eneo hilo kuhamia nyanda za juu ili kuepuka hasara inayochangiwa na mafuriko hayo.

“Leo tuko hapa Lumshi na tutazunguka Chalaluma na viunga vyake kuzisaidia familia zilizoathiriwa na mafuriko kwa chakula, dawa, vyandarua na misaada mingine. Kaunti ikishirikiana na wahisani wengine tutajitahidi kuona kwamba hakuna familia hata moja iliyoathiriwa na haya mafuriko inaachwa nje,” akasema Bw Timamy.

Waziri wa Afya Kaunti ya Lamu, Dkt Mbarak Bahjaj alisema tayari familia 12 ambazo zilikuwa na wagonjwa maeneo ya mafuriko zimefikiwa na kusaidiwa kwa matibabu.

“Kati ya familia hizo 12 zilizofikiwa, tulipata mgonjwa ambaye hali yake ilikuwa mbaya. Tulimbeba na kumtafutia matibabu zaidi na kwa sasa hali yake inaendelea kudhibitiwa,” akasema Dkt Bahjaj.

Kwa upande wake, Mshirikishi wa Msalaba Mwekundu Ukanda wa Pwani, Hassan Musa alisema huenda idadi ya familia zilizoathiriwa na mafuriko Lamu na Pwani kwa ujumla ikaongezeka kadri siku zinavyosonga.

“Kweli tumefikisha misaada, ikiwemo unga wa ngano na mahindi, mafuta ya kupikia, vyandarua na vinginevyo lakini ninahofia hali ikiendelea hivi, hasa Lamu, familia 369 zilizoathiriwa kwa sasa huenda zikaongezeka,” akasema Bw Musa.

  • Tags

You can share this post!

Mama mkwe wa Maina Njenga azirai akilishwa kiapo kortini

Familia yaomba isaidiwe kutafuta mwili wa jamaa aliyezama...

T L