• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Mswada bungeni kubuni ‘mwakilishi-wazee’

Mswada bungeni kubuni ‘mwakilishi-wazee’

Na DAVID MWERE

MSWADA unaopendekeza kuteuliwa kwa mwakilishi wa wazee na kufutiliwa mbali kwa wadhifa wa wawakilishi wanawake ni kati ya miswada itakayoshughulikiwa wabunge watakaporejea kutoka likizoni mwezi Agosti.

Mswada wa Marekebisho ya Katiba 2019 unaofadhiliwa na Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Uasin Gishu, Gladys Shollei, unalenga kuhakikisha jinsia moja haizidi theluthi mbili katika Seneti na Bunge la Kitaifa.

Mswada huo ambao uliwasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni Julai 2019, unapendekeza wanawake watengewe viti 179 ambapo watachaguliwa katika maeneobunge.

Bi Sholei anataka Kifungu cha 98 cha Katiba kifanyiwe marekebisho na kuongeza idadi ya maseneta wanaochaguliwa kutoka 47 hadi 94.

Mbunge huyo wa Uasin Gishu anataka kila kaunti iwe ikichagua maseneta wawili; mwanamke na mwanaume.

Mswada huo pia unapendekeza kuwa vyama vya kisiasa vitateua maseneta sita maalum. Maseneta wanne watawakilisha walemavu na wawili watakuwa wawakilishi wa vijana na wazee.

Kwa sasa, Bunge la Seneti lina jumla ya maseneta 67; maseneta 47 waliochaguliwa na maseneta 16 maalum wa kike na wawakilishi wa walemavu na vijana.

Miswada yote ambayo imekuwa ikiwasilishwa kwa lengo la kutaka pawepo usawa wa kijinsia bungeni, imekuwa ikitupiliwa mbali.

Mswada huo wa Shollei unalenga kufanyia mabadiliko Kifungu cha 97 cha Katiba ili kuongeza idadi ya wanawake wanaochaguliwa katika maeneobunge hadi 136.

Mswada huo pia unapendekeza kuwa idadi ya wanawake wanaoteuliwa katika Bunge la Kitaifa iongezwe kutoka 12 hadi 22.

Bi Shollei anataka maeneobunge mawili yachague mbunge mmoja. Kwa mfano, Kaunti ya Kakamega iliyo na maeneobunge 12 itatoa wabunge sita wa kike.

Katika Kaunti ya Nairobi iliyo na maeneobunge 17, kila maeneobunge mawili yatachagua mbunge mmoja wa kike; na maeneobunge matatu yanayosalia yatachagua mbunge mmoja. Ili mswada huo wa Bi Shollei kupitishwa, utahitaji kura ya maamuzi kwani unahusu ugatuzi.

You can share this post!

Talaka ya Uhuru na Ruto baraka kwa Tanzania

Biden aipapura Facebook kutozima habari za uongo kuhusu...