• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
Obure ahusisha Mudavadi na kashfa ya Anglo-Leasing

Obure ahusisha Mudavadi na kashfa ya Anglo-Leasing

Na RICHARD MUNGUTI

KINARA wa Chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi aliidhinisha mradi wa Anglo-Leasing uliosababisha serikali kupoteza mabilioni ya pesa, Waziri wa Fedha wa zamani, Chris Obure aliambia mahakama ya kuamua kesi za ufisadi jana Jumatano.

Akijitetea katika kesi ya ubadhirifu wa Sh1.2b katika sakata ya Anglo-Leasing, Bw Obure alisema, Mudavadi ndiye alimwandikia barua alipe kampuni moja ya Amerika iliyokuwa inaimarisha huduma za posta.

Bw Obure ambaye ni waziri msaidizi katika wizara ya uchukuzi alimweleza hakimu mkuu Bi Anne Mwangi, kwamba, “alifahamishwa kwa mara ya kwanza kuhusu mradi wa Anglo-Leasing na Mudavadi alipoomba idhini ya kuwasiliana moja kwa moja na kampuni hiyo ya Amerika.”

Bw Obure aliyepatikana na kesi ya kujibu katika sakata hiyo ya Anglo-Leasing alisema Mudavadi alimsihi aidhinishe matumizi ya zaidi ya Sh900milioni katika mradi huo wa kuimarisha utenda kazi wa Shirika la Posta (PCK).

Mahakama ilifahamishwa Mudavadi alimweleza Obure mradi huo wa kuimarisha huduma za posta ungelifaidi posta zaidi ya 900 kote nchini.

Bw Mudavadi alimweleza Obure mradi huo wa kuboresha huduma za posta ulikuwa uchukue muda wa miaka 10 na alitaka wizara ya fedha iufadhili.

“Bw Mudavadi alinisihi niidhishe mradi huo kwa vile ulikuwa mradi wa Serikali,” Bw Obure alieleza mahakama.

Akijibu maswali kutoka kwa wakili Chacha Odera anayemtetea katika kesi hiyo aliyoshtakiwa pamoja na Katibu mkuu wa zamani Sammy Kyungu na Bw Samuel Bundotich, Bw Obure alisema Bw Mudavadi alimpelekea hati za kandarasi hiyo na kampuni ya Spacenet ya Amerika aziidhinishe.

Bw Obure alisema Mudavadi alimshawishi amruhusu afanye mashauri ya moja kwa moja na kampuni hiyo kwa vile mradi ulikuwa wa Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano.

Bw Mudavadi ndiye alikuwa Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wakati huo Mei, 2002.

“Ulihusika kwa njia gani katika mradi wa Anglo-Leasing,” Bw Odera alimwuliza Bw Obure.

“Nilihusika katika mradi huu nilipoombwa na Bw Mudavadi aliyekuwa waziri wa uchukuzi na mawasiliano nitie sahihi kandarasi ya kuboresha huduma za posta nchini,” alijibu Bw Obure.

Mahakama ilifahamishwa, Mudavadi alikuwa amesema huduma hizo zikiboreshwa walimu, polisi, wahudumu wa posta na watumishi wa umma watafaidika kwa vile mishahara itakuwa inatumwa moja kwa moja.

Baada ya kupokea hati za kandarasi hiyo alizipeleka kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Amos Wako na kuziidhinisha.

Na wakati huo huo, Bw Kyungu alisema aliidhinisha matumizi ya pesa hizo baada ya mradi wa Anglo-Leasing kukubaliwa na serikali.

Kesi inaendelea leo Alhamisi.

You can share this post!

Kinaya cha Kenya tajiri bila senti mifukoni

Kenya kunufaika kupitia mpango wa FAO kukabili athari za...

T L