• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Poland na Mexico watoshana nguvu katika Kundi C baada ya Lewandowski kupoteza penalti

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Poland na Mexico watoshana nguvu katika Kundi C baada ya Lewandowski kupoteza penalti

Na MASHIRIKA

KIGOGO Robert Lewandowski alipoteza mkwaju wa penalti katika mchuano wa Kundi C ulioshuhudia timu yake ya taifa ya Poland ikiambulia sare tasa dhidi ya Mexico ugani 974 Stadium.

Lewandowski ambaye hajawahi kufunga bao katika makala yote mengine ya awali ya fainali za Kombe la Dunia, sasa atasubiri zaidi kucheka na nyavu baada ya juhudi zake kuzimwa na kipa mzoefu wa Mexico, Guillermo Ochoa, 37.

Mvamizi huo wa zamani wa Bayern Munich hakubahatika kufunga bao lolote katika fainali za 2018 nchini Urusi dhidi ya Senegal, Colombia na Japan katika Kundi H.

Uwanja wa 974 Stadium, ambao una uwezo wa kubeba 40,000 walioketi, ulikuwa na idadi kubwa ya mashabiki wa Mexico waliosisimka na kuanza kushangilia kila tukio baada ya mkwaju wa Lewandowski kupanguliwa na Ochoa.

Hali hiyo ilichochea zaidi motisha ya Mexico waliopoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Alexis Vega, Hirving Lozano na Jorge Sanchez waliomtatiza pakubwa kipa wa Poland, Wojciech Szczesny.

Matokeo ya mechi hiyo kati ya Poland na Mexico yalisaza Saudi Arabia kileleni mwa Kundi C kwa alama tatu baada ya kutoka nyuma na kuduwaza Argentina kwa ushindi wa 2-1 katika mchuano mwingine wa kundi hilo.

Lewandowski, 34, anajivunia mabao 18 kutokana na michuano 19 ambayo amesakatia Barcelona msimu huu wa 2022-23. Alipewa penalti dhidi ya Mexico baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kuwa alichezewa visivyo na Hector Moreno ndani ya kijisanduku.

Sare dhidi ya Mexico inamaanisha kuwa Poland wameshinda mechi moja pekee kati ya tisa zilizopita kwenye ufunguzi wa kampeni za Kombe la Dunia. Makala ya mwaka huu nchini Qatar yanawapa fursa nzuri ya kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza tangu 1986.

Kwa upande wao, Mexico wanajivunia rekodi ya kufuzu kwa hatua ya 16-bora kwenye makala manane yaliyopita ya fainali za Kombe la Dunia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Saudi Arabia yaduwaza dunia baada...

Mihadarati yasukuma vijana wengi gerezani

T L