• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
‘Shetani’ aingia kanisani na kutawanya na kujeruhi waumini

‘Shetani’ aingia kanisani na kutawanya na kujeruhi waumini

NA TITUS OMINDE

KULITOKEA kizaazaa katika kanisa moja katika wadi ya Kipkenyo viungani mwa mji wa Eldoret baada ya kiongozi mmoja wa kisiasa kuingia ndani ya kanisa akiandamana na kundi la vijana na kutangaza kuwa shetani amewasili kanisani humo.

Kwa mujibu wa wazee wa kanisa hilo, ni kwamba kiongozi huyo pamoja na vijana wake walisambaratisha ibada huku waumini wakitoroka kutokana na hofu ya kuvamiwa na vijana hao.

Hatua ya mwanasiasa huyo ilichochewa na mzozo wa umiliki ardhi kati yake na kanisa hilo ambapo waumini wa kanisa hilo wanadai kuwa, kiongozi huyo anatumia nguvu kuwapokonya ardhi yao kwa madai ya kutaka kujenga shule ya umma katika ardhi hiyo.

“Tangu Jumapili, Mei 16, 2023 waumini wetu wameingiza baridi kutokana na kile walichoshuhudia baada ya kiongozi mmoja wa kisiasa kutoka katika bunge la kaunti ya Uasin Gishu kutuvamia akijiita shetani huku wafuasi wake wakipiga waumini wetu,” alisema Mzee Philip Rono ambaye ni mmoja wa wazee wa kanisa la Kimosong AIC.

Mzee Rono alisema licha ya kuripoti tukio hilo katika kituo cha polisi, hakuna hatua yoyote ambayo imechukuliwa.

Kwa muujibu wa wazee hao ni kwamba tangu tukio hilo, idadi ya waumini imepungua kutokana na hofu na kumbukumbu ya mkasa huo.

Baadhi ya wazee ambao walijeruhiwa wakati wa vurugu hiyo wameandikisha taarifa kwa polisi baada ya kutibiwa hospitalini.

Wazee husika wanadai kuwa licha ya kuwepo kwa agizo la mahakama kuzuia MCA kuingilia shughuli za kanisa hilo hadi kesi ya kupinga kutwaliwa kwa ardhi yao isikilizwe na kuamuliwa, wangali wanasumbuliwa.

Wazee hao wanadai kuwa kiongozi huyo amepuuza agizo la mahakama huku akidai kuwa yeye ni zaidi ya mahakama.

“Tuko na agizo la mahakama kumzuia kuingilia shughuli zetu lakini bado alipuuza agizo hilo. Tayari ametenga ardhi ya kanisa na kujiwekea ua hata kabla ya kesi iliyoko mahakamani kusikilizwa na kuamuliwa,” alisema Mzee Joseph Maina kutoka kanisa hilo.

Tayari kamishna wa kaunti ya Uasin-Gishu Edyson Nyale amepokea malalamishi ya wazee hao na kutoa ahadi kuwa sheria itafuatwa kutafuta ukweli kuhusu madai hayo.

“Hakuna mtu ambaye ana ruhusa ya kuingilia ardhi ya kanisa na kudai kuanzisha shule ya umma bila kufuata utaratibu wa kisheria. Madai ya kanisa hilo yatachunguzwa na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya washukiwa,” alisema Bw Nyale.

Juhudi za kuzungumzwa na diwani wa Kipkenyo David Letting ambaye analaumiwa na waumini wa kanisa hilo hazikufaulu.

Tukio hilo limelaaniwa na afisa mkuu kutoka shirika la haki za kibinadamu la CAT Bw Kimtai Kurui ambaye alitishia kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na diwani huyo katika bunge la kaunti ya Uasin-Gishu.

“Si vyema kwa kiongozi ambaye alichaguliwa kusaidia wanyonge kuendelea kutatiza amani na kunyakua ardhi bila kuzingatia sheria. Kama mashirika ya kibinadamu tutawasilsha bungeni hoja ya kutokuwa na imani na mshukiwa ambaye ni mwakilishi wa wadi wa eneo hili,” alisema Bw Kurui.

  • Tags

You can share this post!

Maombi ya kitaifa: Mbunge Silvanus Osoro ni gwiji katika...

Mswada wa Fedha: Mikakati ya Azimio kuuzima imeiva

T L