• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
SOLAI: Aibu kwa maafisa wa serikali kujinufaisha na misaada ya waathiriwa

SOLAI: Aibu kwa maafisa wa serikali kujinufaisha na misaada ya waathiriwa

Na MAGDALENE WANJA

Miezi minane baada ya mkasa wa bwawa la Solai kutokea, maswali yanaendelea kuibuka mwaka ukiisha kuhusu kama ilikuwa ajali ama kosa la kibinadamu.

Waathiriwa wa janga hilo ambalo liliwaangamiza watu 48 bado wamesalia katika hali ya duni huku janga hilo likiacha alama ya kudumu katika maisha yao.

Kuna waathiriwa waliopoteza jamaa zao huku wengine wakipoteza mali kutokana na mkasa huo.

Kabla ya tukio hilo, vijiji vya Energy na Nyakinyua vilikuwa kama vijiji vingine nchini ambapo shughuli kuu ilikuwa ukulima na biashara za rejareja.

Hii ilibadilika usiku huo baada ya tukio hilo kufanyika na sasa eneo hilo limesalia kuwa kivutio cha watalii wa aina mbalimbali.

“Kuna aina mbalimbali ya watu ambao bado hulitembelea eneo hili kujionea yaliyotokea miezi nane baadaye wakiwemo maafisawa serikali, mashirika  na watu binafsi,” alisema mkazi mmoja wa Solai.

Maafisa wa serikali wakikagua eneo la mkasa. Picha/ Maggy Wanja

Kufikia leo uharabifu uliofanyika unaonekana wazi zikiwemo nyumba, barabara na baadhi ya watu waliobakia na majeraha.

Ata hivyo, wanasiasa walichukua nafasi hiyo na kulifanya eneo hilo kuwa jukwaa la kisiasa la kujipigia debe.

Hii ni licha ya kuwa wakazi hao walikuwa wanaendelea kuomboleza wapendwa wao huku tumaini lao la pekee likisalia kwa mikono ya wasamaria wema.

Migawanyiko ya kisiasa ilionekana kwa uwazi huku baadhi ya maafisa wa serikali wakishutumiwa kuwa walijinufaisha na misaada iliyotolewa kwa waathiriwa.

Kulingana na mwakilishi wa wadi ya eneo hilo Bw Peter Mbae, juhudi za waathiriwa hao za kutaka kukutana na wamiliki wa bwawa hilo hazikufua dafu.

“Kupitia kwa wakili wa familia hiyo, Bw Patel alisema kuwa alikuwa tayar kukutana na waathiriwa mahakamani,” alisema Bw Mbae.

Bw Mbae alisema kuwa, ijapokuwa familia ya Patel imekuwa jirani ya waathiriwa kwa zaidi ya miongo miwili, wamesalia bila namna nyingine ya kudai haki yao.

Bwawa la Solai lililomeza watu 48. Picha/ Maggy Wanja

“Tumekubaliana kwamba tutaenda mahakamani mwezi Januari 2019 ili kuitaka familia hiyo kuwalipa waathiriwa fidia,” akasema Bw Mbae.

Mnamo mwezi Juni,kamati ya bunge ya mazingira na rasili mali asili ilitembelea shamba la Milment Solai ambako linamilikiwa na familia ya Patel ila hawakufankiwa kupata jawabu lolote kwani wasimamizi wake hawakutoa stakabadhi zozote.

Kamati hiyo ikiongozwa na naibu mwenyekiti Bi Sophia Abdi ilifanya mkutano na wasimamizi wa shamba hilo pamoja na viongozi wa kaunti ya Nakuru ila hawakufanikiwa kupata habari yoyote.

Mwezi huo huo, kamati ya seneti ikiongozwa na mwenyekiti wake seneta Mutula Kilonzo ilitembelea shamba hilo na kuchukua ripoti.

Kufikia sasa, hakuna ripoti yoyote ambayo imetolewa na kamati zote zilizotembelea eneo hilo.

You can share this post!

KRISMASI: Mamia wakwama

Swazuri aonywa vikali dhidi ya kuvuruga ushahidi

adminleo